Jumamosi, 9 Machi 2019

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU YATAKIWA KUBORESHA MIFUMO YA UOMBAJI MIKOPO

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. William Ole Nasha ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu  (HESLB) kuweka mifumo itakayowezesha vijana wengi kuomba mikopo ya kuwaendeleza kitaaluma kiurahisi.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo alipofanya kikao na watumishi wa Bodi hiyo jijini Dar es Salaam ambapo amesema kumekuwa na changamoto katika ujazaji wa fomu za maombi ya mikopo na kupelekea wengi kukosa mikopo hiyo.

"Bodi imekuwa ikifanya kazi nzuri sana katika suala zima la utoaji na ukusanyaji wa mikopo lakini  kuna changamoto katika ujazaji wa fomu za maombi ya mikopo wengi wanakosea sijui ni tatizo la taarifa ama elimu" amehoji Naibu Waziri.

 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Wiliam Ole Nasha akiongea na watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wakati wa kikao na watumishi hao ambapo amewaagiza kuweka mifumo rafiki ya uombaji mikopo ili kuwezesha vijana wengi zaidi kuomba mikopo.

Ole Nasha ameitaka Bodi hiyo kuendelea kutoa elimu na taarifa kwa umma kuhusu namna bora ya ujazji wa fomu hizo ili kupunguza changamoto hiyo na kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kupata lakini na kuongeza ufanisi katika shughuli za kiutendaji katika Bodi.

Amesema pamoja na changamoto hiyo pia zipo changamoto kwa baadhi ya Maafisa mikopo katika vyuo ambao wamekuwa wakijifanya miungu watu jambo ambalo limekuwa likichelewesha upatikanaji wa mikopo kwa wanaostahili na kupelekea lawama kupelekwa kwa Bodi hiyo.

"Ni vyema pia kuangalia namna bora ya kuwapata Maafisa Mikopo katika vyuo kwani nao ni sehemu ya tatizo katika kutoa mikopo, kuna wengine wanawadai wanavyuo fedha ili washughulikie maombi yao" amesema Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Wiliam Ole Nasha akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wakati wa kikao na watumishi hao.

Aidha, Naibu Waziri Ole Nasha ameipongeza  bodi kwa kufanya kazi nzuri katika urejeshaji wa Mikopo kwa kukusanya zaidi ya Sh.Bilioni 108 katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019 ambapo lengo lilikuwa ni kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 150 kwa mwaka 2018/19.

Awali Mkurugenzi wa Habari wa Bodi ya Mikopo Omega Ngolle alimweleza Naibu Waziri kuwa changamoto zinazokwamisha ama kuchelewesha utoaji wa mikopo ni kwa baadhi ya taasisi kuchelewa kuwasilisha taarifa za matokeo au kutoa taarifa zisizo sahihi kwa Bodi hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.