Ijumaa, 4 Oktoba 2019

WAZIRI NDALICHAKO AWAASA WANAFUNZI WANAOMALIZA KIDATO CHA NNE KUWA NA MAADILI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako  amesema elimu bila nidhamu na maadili haiwezi kusaidia kufanikiwa katika maisha.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo wakati wa mahafali ya 32 ya shule ya sekondari Suji iliyoko  wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Amesema katika maisha ili mtu afanikiwe ni lazima awe na nidhamu ya kufanya kazi aliyonayo kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuheshimu mamlaka na hata watu walio chini yako na kuwataka wanafunzi  kuyaishi hayo mara baada ya kumaliza elimu ya kidato cha nne
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akimtunuku cheti cha kuhitimu kidato cha Nne Mwanafunzi Tajiel Omary wa Shule ya Sekondari Suji iliyoko wilayani Same Mkoani Kilomanjaro

Kiongozi huyo ameupongeza uongozi wa shule ya sekondari Suji kwa kuwalea wanafunzi katika maadili mema ya kumjua Mungu na kuwapongeza kwa  kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha nne na cha sita.
Ndalichako amewataka wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yao ili wengi zaidi waweze kufaulu kwa kupata daraja la kwanza.

"Pamoja na ufaulu wenu mzuri lakini nataka  daraja la kwanza ziongezeke, kwa sababu ukiangalia matokeo ya shule hii kwa miaka mitatu  mfululizo kuanzia 2016 hadi 2018 hata kama hakuna daraja la nne lakini wanaopata daraja la kwanza ni wachache hivyo ongezeni juhudi ili ili huku kwenye daraja la kwanza muongezeke,"alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa mahafali ya 32 ya Shule ya Sekondari Suji iliyoko Wilayani Same mkoani kilimanjaro

Amewataka wanafunzi kuwa na uzalendo na nchi yao ikiwa ni pamoja na kuzilinda tunu Taifa zilizoachwa na waasisi waxtaifa letu  ambazo ni pamoja na amani, umoja na  mshikamano.

"Mnaona kazi kubwa ambayo Rais wetu wa Awamu ya Tano  anaifanya anahakikisha rasilimali za nchi haziibiwi zinawanufaisha watu wote hivyo mnapomaliza mkamuunge mkono kwa kufanya kazi kwa bidii ili dhamira yake ni kuona nchi yetu inapata maendeleo inafanikiwa ," alisema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuwatakia heri na mafanikio wanafunzi wote wa kidato cha nne wanaotarajia kuanza mitihani yao Mwezi Novemba mwaka huu.
Baadhi ya wahitimu wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Suji ya Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro wakiingia kwenye mahafali yaliyofanyika katika viawanja vya shule hiyo

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same Rozimary Staki amesema Wilaya ya same ina shule za sekondari 53 ambapo 17 zinamilikiwa na watu binafsi pamoja na taasisi za dini.

Staki amesema kama Wilaya wamekuwa wakishirikia na na Viongozi wa Dini katika kuelimisha mabinti umuhimu wa kujitambua wanapokuwa shuleni.

Nae Mkuu wa Shule ya Sekondari Suji Silnani Dismas amesema shule hiyo pamoja  na kusisitiza masoma inawalea  wanafunzi katika maadili na nidhamu ya hali ya juu  kwa kuwa ni ya kanisa.

Dismas amesema shule hiyo ina wanafunzi takribani 568 na mafanikio wanayojivunia ni kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akisalimiana na Walimu wa shule ya Sekondari Suji mara baada ya kuwasili katika shule hiyo kwa ajili ya mahahafali ya 32 ya shule hiyo.

Mwanafunzi bora katika masomo Tajiel Omary ambae anatarajia kuhitimu masomo ya kidato cha nne mwaka huu amasema ufauli katika masomo unatokana na juhudi ambazo amekuwa akizifanya katika masomo ikiwa ni pamoja na kumuomba Mungu ili malengo yake yatimie. 

Waziri Ndalichako pia alitembelea shule ya sekondari Makanya na kuongea na wanafunzi ambapo amewatakia pia heri katika mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne Mwezi Novemba mwaka huu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akifurahi pamoja na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Makanya iliyopo Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni