Jumamosi, 21 Desemba 2019

BILIONI 37 KUJENGA TAASISI YA TEKNOLOJIA DAR ES SALAAM (DIT) KAMPASI YA MWANZA

Serikali imezindua mradi wa ujenzi wa majengo mapya yenye thamani ya Sh. Bilioni 37 katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia (World Bank).

Uzinduzi huo umefanywa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha alipomuwakilisha Waziri wa wizara hiyo kwenye mahafali ya kwanza ya Taasisi hiyo katika kampasi ya Mwanza ambapo amesema ujenzi huo utaanza karibuni na unatarajiwa kukamilika Desemba 2024.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akihutubia hadhira iliyoshiriki katika mahafali ya  kwanza ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza.
Ole Nasha ameongeza kuwa mradi huo utaongeza udahili kwa zaidi ya asilimia 50 katika fani mbalimbali za ufundi na teknolojia na utawezesha kuhuisha mitaala katika fani ya ngozi ili kuzalisha mafundi mahiri watakaoweza kujiajiri na kuajiriwa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akipewa maelezo ya mchoro unaoonesha majengo yatakavyokuwa baada ya kukamilika kwa Mradi wa Ujenzi mwaka 2024. Anayetoa maelezo hayo ni Mkurugenzi wa DIT kampasi ya Mwanza, Dkt. Albert Mmari.
Waziri Ole Nasha pia ametoa rai kwa wanafunzi waliopata mikopo kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii na kujiepusha na vurugu  kwani zinaweza kuwaletea matatizo ikiwemo kuchukuliwa hatua na kukosa fursa za mikopo.

"Wanafunzi waliopata mikopo wajione kuwa wana bahati sababu kati ya wanafunzi zaidi ya elfu 70 wa mwaka wa kwanza walioomba ni 49,485 ndio waliopata, kwahiyo mnapopata fursa ya mkopo muitumie vizuri kwa kusoma na kujiongezea elimu kwa ajili ya maisha yenu ya baadaye na taifa kwa ujumla," amesisitiza Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa ujenzi wa majengo mapya katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Prof. Apollinaria Pereka akisoma historia ya DIT kampasi ya Mwanza amesema taasisi hiyo ilikidhi vigezo vya usajili wa kudumu kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) mwaka 2016 na kupewa kibali cha kuanzisha kozi ya teknolojia ya ngozi na sayansi na teknolojia ya maabara katika ngazi ya Stashahada.

Amesema anaamini DIT kampasi ya Mwanza itatekeleza azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhakikisha inatoa wataalamu ambao wataifikisha nchi katika uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo mwaka 2025.

Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 11 wametunukiwa Stashahada ya sayansi na teknolojia ya maabara, wakiwemo wasichana wanne na wavulana saba.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akimtunuku cheti mmoja wa wahitimu wa Stashahada ya sayansi na teknolojia ya maabara katika mahafali ya kwanza ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa Stashahada ya sayansi na teknolojia ya maabara waliotunukiwa vyeti katika mahafali ya kwanza ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Mwanza.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni