Jumatano, 26 Mei 2021

Vyuo Vikuu vyahimizwa kufanya tafiti zenye tija kijamii na kiuchumi

 Vyuo Vikuu nchini vimehimizwa kujikita katika tafiti na bunifu endelevu zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali za jamii pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi.


Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.Leonard Akwilapo kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Profesa Joyce Ndalichako wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Sita ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Amesema kuwa vyuo hivyo vinatakiwa kufanya tafiti zitakazoweza kujitofautisha na taasisi zingine za elimu na kwamba zilenge katika kuisaidia jamii kupunguza changamoto na kuleta maendeleo.

" Vyuo Vikuu lazima vifanye tafiti za kuilenga jamii visipofanya vitakuwa havina utofauti na shule za kawaida tafiti ziibue majibu kusaidia nchi kimaendeleo," amesema Dkt. Akwilapo.

Amebainisha kuwa tafiti zinazofanywa na vyuo vikuu huvisaidia kujiweka karibu na jamii pamoja na kujitangaza kimataifa kwani matokeo ya tafiti husambazwa sehemu mbalimbali.

Amekipongeza chuo hicho kwa kuandaa maadhimisho hayo kwa kutenga fedha zake za ndani huku kwani kinaonyesha dhahiri kilivyojipanga kutatua kero za jamii na kuchochea maendeleo ya viwanda.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema maadhimisho ya kilele cha wiki hiyo yamelenga kuonyesha jinsi gani UDSM haijajitenga na jamii kupitia tafiti na bunifu zilizowasilishwa.

Amesisitiza kuwa wiki hiyo ni kiungo muhimu kati ya chuo na umma huku akiwapongeza washindi na walioshinndwa kuendelea kutafuta kuendelea kutafuta mawazo mengine ya utafiti na ubunifu.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Utafiti wa chuo hicho Profesa Bernadeta Killian amesema maadhimisho hayo yalianza mwaka 2015 na sasa yanejikita katika kuhimiza rafiki za kiuchumi kulingana na uhitaji katika kukuza uchumi wa Nchi kupitia Viwanda. 

Katika kilele hicho tuzo na hundi za fedha taslimu zilizotolewa ikiwemo ya Jarida bora la mwaka 2021, Tuzo ya Idara iliyoleta fedha nyingi za utafiti chuoni hapo ilikwenda kwa Shule ya Biashara iliyoleta Sh Bil 2.5,  tuzo ya Mtafiti hodari wa mwaka 2021 imechukuliwa na Dkt.Samwel Lyimo na 

Tuzo ya Mbunifu hodari amepta Dkt.Budeba kutoka Chuo cha Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam DUCE.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni