Serikali
imeendelea kuongeza ubora wa elimu na kukuza ujuzi ili kuongeza tija katika
uzalishaji na kuongeza ajira nchini. Hii imewezekana kwa kuweka sera,
mifumo na miundo mbinu wezeshi kwa watanzania kuweza kupata ujuzi na umahiri
unaohitajika katika kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya mpango wa
maendeleo 2025 na malengo endelevu ya milenia.
Kauli
hiyo imetolewa Jiji Arusha na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Profesa Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa tatu wa
Kimataifa wa Nishati endelevu na Teknolojia ya maji (International Conference
on Energy, Aquatech and Sustainability 2019, ICEAS) )wenye lengo la kujadili
changamoto zinazokabili sekta ya Nishati hususan kukuza nishati
mbadala na Teknolojia ya Miundombinu ya maji na kuja na mapendekezo ya
namna bora ya kutumia rasimali zilizopo katika jamii kukuza sekta hizo.
Amesema
lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inajenga uchumi wa viwanda ni
kuhakikisha kuwa elimu itolewayo inakuwa bora na kuendeleza ujuzi kwa
watanzania ili waweze kuongeza thamani katika mazao kutumia teknolojia ya
kisasa, ambapo maji na nishati ni maeneo muhimu katika kutekeleza hili.
"Tunataka
kuona kama ni mkulima anakuwa na uwezo wa kuongeza thamani ya mazao kwa
kutumia Teknolojia za kisasa na hasa kutumia tafiti zilizofanywa,"
alisema Waziri Ndalichako
Baadhi wa wajumbe wa Mkutano wa ICEAS wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa mkutano huo jijini Arusha. |
Katika
hatua nyingine Waziri Ndalichako ameipongeza Taasisi ya Sayansi na Teknolojia
ya Nelson Mandela (NM-AIST) kwa kuboresha kiwango cha utafiti katika chuo
hicho ikiwa ni pamoja na programu wanazotoa.
"Mwaka
2017 hapa NM-AIST tumefanya uzinduzi wa vituo vinne vya umahiri vya Sayansi na
Teknolojia katika elimu ya juu kwa lengo la kuhakikisha tunaboresha elimu yetu
na kunakuwa na wigo mpana wa kufanya tafiti, tunaona sasa mnafanya vizuri na
kuendana na moto wa Chuo ambao ni Taaluma kwa jamii na viwanda, na hata maji ya
kunywa yanayotumika katika mkutano huu ni moja ya kazi za tafiti zinazofanyika
hapa"aliongeza Waziri Ndalichako
Waziri
Ndalichako kabla ya kutoa hotuba yake ametumia fursa hiyo kutuma salamu za pole
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,
ndugu jamaa na marafiki kufuatia vifo vya watanzania vilivyosababishwa na ajali
ya moto jijini Morogoro Agosti 10, 2019.
Naye
Makamu Mkuu wa Chuo katika Taasisi ya Sayansi Teknolojia ya Nelson Mandela
ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa ICEAS Profesa Emmanuel Luoga amesema
mkutano huo umewaleta pamoja wataalamu wa nishati mbadala na endelevu na
watafiti kutoka nchi mbalimbali ambapo mada 37 zitawasilishwa wataalamu
kutoka nchi 11 zilizoshiriki mkutano huo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akibadilishana mawazo na mmoja wa wajumbe wa mkutano wa ICEAS Jijini Arusha. |
Mada
zitakazojadiliwa zitajikita katika maeneo ya mabadiliko ya tabia nchi,
upatikanaji wa maji, nishati mbadala na endelevu.
Aidha
amesema Taasisi anayoingoza itaendelea kushirikiana na taasisi na vyuo vingine
kutoka ndani na nje ya nchi kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto
mbalimbali za kijamii pamoja na kuendeleza viwanda.