Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya
Bukoba, Morris Limbe kumlipa fedha Mkandarasi anayekarabati shule ya sekondari Bukoba
ili aweze kuendelea na kazi na kukamilisha ukarabati huo kwa wakati
Naibu Waziri Ole Nasha
ametoa agizo hilo mkoani Kagera wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo
ya sekta ya elimu inayotekelezwa mkoani humo, ambapo amesema Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia ilishapeleka fedha zote za ukarabati huo kiasi cha shilingi
bilioni 1.4 lakini mpaka sasa mkandarasi huyu amelipwa kiasi cha shilingi
milioni 32 tu.
“Fedha zilishaletwa zote na
wizara shilingi bilioni 1.4 lakini mpaka sasa Mzinga wamelipwa shilingi milioni
32 tu kati ya milioni mia mbili na zaidi walizotakiwa kuwa wamelipwa mpaka
sasa, hivyo Mkurugenzi wa manispaa dirisha likifunguliwa hakikisha Mzinga
wanapata fedha ambazo wanadai” amesisitiza Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu
Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akikagua baadhi ya majengo ya shule ya
Sekondari Bukoba ambapo amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba kumlipa
Mkandarasi ili ukarabati uendelee.
Ole Nasha amesema ukarabati wa
shule hiyo unaoendelea umechelewa kukamilika kwani licha ya fedha hizo
kupelekwa mapema mkandarasi amechelewa kuanza kufanya ukarabati huo. Hata hivyo
amesema kasi ya ujenzi huo si mbaya kutokana na kuanza mwezi wa tano.
Aidha, Ole Nasha amewataka
watendaji wa manispaa hiyo kufuatilia kwa ukaribu matumizi ya fedha hizo kwani
ni nyingi kutumika kwa ukarabati ukilinganisha na fedha zinazotumika katika
miradi mingine, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa fedha kubaki na kutumika katika
kufanya shughuli nyingine za kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
“Nikifananisha fedha ambazo
tumetumia kwenye maeneo mengine na miradi mingine mfano miradi ya afya ambao
wanatumia bilioni 1.5 kujenga hospitali kubwa kwa kujenga majengo mapya makubwa
saba lakini sisi hiyo bilioni 1.4 ambayo inakaribiana na bilioni 1.5 ya afya
tunakarabati majengo tu, kuna umuhimu wa kuzisimamia fedha hizi kwa
ukaribu," alisema Ole Nasha.
Aidha, Naibu Waziri amesema
shule hiyo ina nafasi finyu ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanafunzi mia saba
waliopo na amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
Dkt. Leonard Akwilapo kuwasiliana na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) ambao
wana eneo karibu na shule hiyo washaurine juu ya uwezekano wa kutoa eneo hilo
kwa ajili ya upanuzi wa shule hiyo.
Muonekana wa Shule ya
Sekondari Bukoba inayofanyiwa ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia baada ya kuharibiwa na tetemeko la ardhi la mwaka 2016 ambapo baadhi
ya kuta za shule hiyo zilianguka na majengo mengine kupata nyufa na baadae paa
kuezuliwa na upepo mkali.
Shule ya Sekondari ya Bukoba
inafanyiwa ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia baada ya
kuharibiwa na tetemeko la ardhi la mwaka 2016 lililoikumba mkoa wa Kagera
ambapo baadhi ya kuta za shule hiyo zilianguka na majengo mengine kupata nyufa
na baadae paa kuezuliwa na upepo mkali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.