Jumamosi, 10 Agosti 2019

BILIONI 4.6 KUJENGA NA KUKARABATI CHUO CHA UFUNDI KARAGWE

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4.6 kutekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.

Hayo yamesemwa Wilayani Karagwe na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu katika wilaya hiyo, ambapo amesema lengo la kutekeleza mradi huo ni kuongeza udahili wa wanafunzi wanaochukua masomo ya ufundi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta a elimu wilayani humo.
Ole Nasha amesema serikali imeweka mkakati wa kukarabati na kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya, kwani ili kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu kama nchi kuwa na vijana wenye maarifa na stadi mbalimbali za ufundi zitakazowawezesha  kuajiriwa, kujiajiri na kushiriki katika uchumi wa viwanda.


“Rais ameweka nguvu nyingi katika kuinua uchumi wa nchi yetu, mnaona sasa miradi mikubwa inakuja, hospitali zinajengwa, barabara za lami nyingi zinajengwa, kwa hiyo kuna mambo mengi yanafanyika katika ujenzi na miradi yote hii yote yanahitaji ufundi, hivyo mtambue ufundi ni kitu muhimu sasa” ameongeza Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akisikiliza maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
“Rais ameweka nguvu nyingi katika kuinua uchumi wa nchi yetu, mnaona sasa miradi mikubwa inakuja, hospitali zinajengwa, barabara za lami nyingi zinajengwa, kwa hiyo kuna mambo mengi yanafanyika katika ujenzi na miradi yote hii yote yanahitaji ufundi, hivyo mtambue ufundi ni kitu muhimu sasa” ameongeza Ole Nasha.


Wakati huo huo, Naibu Waziri ametoa miezi mitatu kwa wakala wa majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha wanamaliza ujenzi na ukarabati wa chuo hicho, ambapo amesema hajaridhishwa na sababu zilizotolewa na mhandisi msanifu kutoka TBA zilizopelekea kutokamilika kwa mradi kwa wakati.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akizungumza na wanafunzi wa wanaosoma katika Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, ambapo amewasisitiza kusoma kwa bidii na kuwataka kuthamini mafunzo wanayoyapata kwani muhimu katika kujiletea maendeleo na kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi.
Awali Mhandisi Msanifu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Kelvin Joas alimweleza Naibu Waziri kuwa kutokukamilika kwa mradi huo kwa wakati nikutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo za kimkataba na kuwapelekea kuomba kuongezewa muda wa miezi sita  baada ya muda wa mkataba kuisha Julai 26,2019.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Godwini Kitonka amesema Halmashauri yake inaishukuru serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutenga fedha zaidi ya bilioni 4.6 kwa ajili ya kujenga majengo mapya ambayo ni jengo la utawala, ukumbi mdogo, vyoo vya nje, bweni la wasichana na kukarabati karakana ya ushonaji na uchomeleaji chuma.
Baadhi ya majengo yanayojengwa katika Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya yaa Karagwe, ambapo serikali kupitia wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga zaidi ya shilingi bilioni nne kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo katika chuo hicho.
Mwanafunzi Masau Josephat, wameishukuru serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuongeza majengo ambayo awali hayakuwepo, kwani mwanzoni hayakuwa yakiridhisha, huku wakiiomba serikali kuongezea baadhi ya kozi ambazo hazipatikani chuoni hapo ili kupanua wigo wa maarifa na stadi kwa vijana wa Karagwe na maeneo ya jirani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni