Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania inakusudia kufanya maboresho ya
mtaala wa elimu ya ualimu ili iendane na mitaala mipya ya elimu ya Sekondari na
msingi ambayo imeanza kutumika mwaka 2015.
Hayo yamesemwa Jijni Dar es
Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi
wa mkutano wa wadau wa Elimu ya Ualimu ambao wamekutana kwa lengo la kutoa
maoni yatakayosaidia kuboresha usimamizi na maendeleo hususan maboresho ya mtaala
wa elimu ya ualimu.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa ufunguzi wa
Mkutano wa wadau wa Elimu ya Ualimu kuhusu usimamizi na uendeshaji bora wa
Elimu ya Ualimu uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Dkt.Akwilapo alisema mtaala wa mafunzo ya ualimu uliopo sasa ni wa zamani akitolea mfano mtaala wa mafunzo ya ualimu kwa walimu wa diploma ambao ni wa mwaka 2008 huku ngazi ya cheti ukiwa wa mwaka 2009 hivyo kutoendana na mtaala mpya wa elimu msingi ambao unazingatia ufundishaji wa KKK.
“Elimu ni suala la Kitaifa
hivyo serikali haiwezi kujifanya haisikii jamii inasema nini ndio maana kikao
cha wadau kimeitishwa na pia Waziri wa elimu yupo mbioni kuitisha mkutano wa
wadau kwa lengo la kupata maoni ya namna bora ya kuboresha Elimu,”aliongeza Dkt Akwilapo.
Aidha Katibu Mkuu huyo amewataka
wadau hao kutumia mkutano huo kujadili na kutafakari kwa kina mfumo wa
maandalizi ya walimu nchini kwa kuzingatia mada ya Usimamizi na Maendeleo ya
Elimu ya Ualimu, Fursa na Changamoto
pamoja na upimaji na tathmini yake.
“Tumieni mkutano huu vizuri
na mambo mtayakojadili yajikite katika kuona ni namna gani mnaboresha mahiri
zinazohitajika kwa mwalimu, ama mkufunzi, mazingira na miundombinu wezeshi,
uongozi na usimamizi wa mafunzo, upimaji na tathmini ya mafunzo pamoja na
maendeleo endelevu ya mwalimu,” alisisitiza Dkt Akwilapo.
Wadau wa Elimu ya Ualimu
wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau hao uliofanyika
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Mkutano
huo Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa
amesema mkutano huo wa wadau
wa elimu utachochea mabadiliko katika
sekta nzima ya elimu kwani ili kufanikiwa katika sekta hiyo ni lazima kuwe na
ushirikishwaji wa wadau wa elimu.
“Tumekutana kwa ajili ya
kuongelea moyo wa Taifa letu, Elimu ni moyo wa taifa unaposema elimu unapozungumzia
elimu ya ualimu katika kuleta mabadiliko ya sekta nzima ya elimu,” aliongeza
Dkt Mtahabwa.
Dkt Mtahabwa anasema unaweza
kujenga shule nyingi, ukawa na vifaa vya kutosha lakini kama hauna walimu bora
ni kazi bure hivyo tunataka walimu wawe na waledi, wawe kioo cha jamii kuanzia
uvaaji wake, kutembea, kuongea na namna anaivyoishi shuleni na hata kijijini
awe mfano wa kuigwa katika jamii.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa
Mafunzo ya Ualimu Augusta Lupokela akizungumza wakati wa Mkutano wa Wadau wa
Elimu ya Ualimu ambapo amesema matokeo ya Mkutano huo yatasaidia katika
maandalizi ya mpango mkakati wa maboresho ya usimamizi wa mafunzo ya ualimu.
Awali Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Ualimu
kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Augusta Lupokela alimweleza
Katibu Mkuu kuwa mkutano huo, pamoja na mambo mengine umelenga kujadili masula
yanayohusu usimamizi wa mafunzo ya ualimu na kwamba mada zitakazowasilishwa zitahusu
usimamizi na maendeleo ya Elimu ya ualimu, fursa zilizopo pamoja na changamoto.
Aliongeza kuwa matokeo ya mkutano huo ni maandalizi
ya mpango mkakati wa maboresho ya usimamizi wa mafunzo ya ualimu ili kufikia
malengo ya serikali ya kutoa elimu bora ya ualimu.
Wadau
wa Elimu ya Ualimu wakiwa wameshikana mkono huku wakiimba wimbo wa “solidarity”
kuashiria umoja katika utekelezaji wa majukumu ili kufikia malengo mapana ya
kutoa elimu iliyo bora.
Nae Mratibu wa mradi wa Elimu kwa Walimu (TESP) Ignasi Chonya amesema kupitia mradi anaousimamia wamekuwa wakitoa mafunzo kwa walimu kazini na walimu tarajali kuhusu matumzi ya TEHAMA, ualimu kwa vitendo kwa vyuo vyote vya Serikali na binafsi ili kuwajengea uwezo wa namna ya kufundisha kwa vitendo.
Mkutano wa wadau wa Elimu ya Ualimu unafanyika kwa
siku tatu kuanzia Agosti 08, 2019 na umehusisha wadau kutoka Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Taasisi zake, Viongozi na Mameneja wa
shule, vyuo vya ualimu kutoka sekta binafsi, Washirika wa Maendeleo na Wizara
ya Elimu.
Katibu Mkuu Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja
na wadau wa mkutano wa wadau wa elimu ya ualimu baada ya kufungua mkutano huo
jijini Dar es Salaam.
Nivyema mkutano ulivyo itishwa kwani ni kweli kuna umuhimu wa kubadili mtaala wa elimu ili elimu yanayotolewa iendane na mabadiliko ya jamii tuliyo nayo na kumuwezesha muhitimu wa mafunzo ya ualimu kuwa na elimu ya kutosha kwa kutumi fursa pia kutoa elimu kwa vijana wengine kuwa wabunifu ili kuendana na mfumo wa maisha wa sasa na badae. Hivyo elimu ya ujasiriamali pia ni ya muhimu.
JibuFuta