Kaimu
Kamishna wa Elimu Nicholas Bureta
amewataka wadau wa Program ya Maji, Afya na usafi wa Mazingira shuleni kurejea
mipango yao ili kuona jinsi na mbinu ngani itumike katika kukabiliana na
changamoto za miundombinu ya Vyoo, Afya
na usafi wa Mazingira zinazozikabili shule mbalimbali nchini.
Akizungumza
katika uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa huduma ya maji, Afya na usafi wa
mazingira shuleni uliofanyika jijini Dar es Salaam amesema kuwa serikali
imeboresha na kujenga miundombinu ya vyoo kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali ingawa bado kuna
upungufu wa matundu ya vyoo bora, uwepo wa baadhi ya miundombinu isiyo rafiki
na kukosekana kwa maji safi na salama shuleni kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Bureta
alielezea changamoto nyingine ambazo zimekuwa kikwazo katika kuboresha
miundombinu na mazingira ya shule kuwa ni pamoja na jamii kutoshiriki
kikamilifu katika kuchangia ujenzi wa miundombinu ya vyoo na maji. Aidha, aliendelea
kusisitiza kuwa changomoto hizi zimeleta athari kwa wanafunzi ikiwemo watoto wa
kike kushindwa kuhudhuria darasani ipasavyo na kusababisha kushindwa kumudu na kutimiza
malengo yao ya kielimu na wanafunzi kupoteza hadhi ya utu kutokana na ukosefu
wa vyoo.
“Ili
kuharakisha utatuzi wa changamoto hizi,
ni lazima kila mdau kujitoa kikamilifu ili kusaidia kuboresha shule zetu ziweze
kufika katika viwango vinavyostahili kwani naamini uboreshaji wa mazingira ya
shule utaleta hamasa kubwa kwa wanafunzi, walimu na jumuiya yote ya shule na
hatimaye kuinua kiwango cha elimu nchini” alisisitiza Kaimu Kamishna wa Elimu.
Aidha,
amewashukuru wadau wote wa program ya Maji, Afya na usafi wa Mazingira shuleni kwa
ufadhili wao mkubwa katika kuboresha miundombinu ya vyoo shuleni ambapo jumla ya
shule 2490 ziliweza kujengewa vyoo bora pamoja na kuwapatia maji safi na
salama. Aliwataja wadau hao kuwa ni pamoja na Benki ya Dunia, Shirika la
kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Idara ya Kimataifa ya Maendeleo ya
Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) na Water Aid ambao wamewezesha
kujengwa kwa miundombinu hiyo katika baadhi ya shule nchini.
Naye
Mratibu wa Program ya Maji, Afya na usafi wa Mazingira shuleni kutoka Wizara ya
Elimu, sayansi na Teknolojia Theresia Kuiwite amesema Program hiyo ilianzishwa baada
ya utafiti uliofanyika mwaka 2009 katika mikoa kumi na mbili ambapo matokeo
yalionyesha kati ya shule 2997 ni asilimia kumi na moja tu ya shule zilikuwa na
vyoo vilivyofikia viwango vinavyohitajika na asilimia sitini na tisa za shule
hazikuwa na huduma ya maji. Aidha, shule zote hazikuwa na miundombinu vya vyoo
kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum.
Kuiwite
anasema program hii imewezesha kuwekwa kwa mikakati ya kuboresha miundombinu
hiyo. Mikakati hiyo ndo ilipelekea kuwepo kwa umuhimu wa kuwa na Mwongozo wa
Kitaifa wa namna gani miundombinu ya vyoo inapaswa kuwa.
“Leo
hii tunazindua Mwongozo wa Kitaifa wa huduma ya maji, Afya na usafi wa
mazingira shuleni ili kuwezesha shule zote nchini kuwa na miundombinu iliyo
bora na salama kwa ajili ya watoto wetu na kuwawezesha kuwa na mazingira bora
kwa ajili ya kufundishia na kujifunza”
alisema mratibu huyo.
Kuiwite
anasema toka kuanza rasmi kwa program mwaka 2011 mpaka sasa shule 2500 zimeweze
kujengewa na kuboreshewa miundombinu bora ya vyoo, yenye vyumba vya watoto wenye mahitaji
maalum, na vyumba vya kujihifadhi vya watoto wa Kike wanapokuwa katika siku za hedhi.
Program
hii unaendeshwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Maji na
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee ambao ni
watekelezaji wakuu wa Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira.