Ijumaa, 24 Aprili 2020
Alhamisi, 23 Aprili 2020
NAIBU WAZIRI OLE NASHA AWAPONGEZA WABUNGE KUJENGA SHULE YA WASICHANA
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha amefanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa
shule maalum ya wasichana inayojengwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika Kata ya Kikombo wilayani Chamwino Jijini Dodoma
Kiongozi huyo amesema lengo la ziara
hiyo pamoja na mambo mengine ni kuona maeneo ambayo Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia itaweza kuchangia ili kukamilisha ujenzi wa shule hiyo katika muda
uliopangwa.
Naibu waziri Ole Nasha amewapongeza wabunge
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kujenga shule
ya wasichana kwani kumuelimisha mtoto wa kike ni sawa na kuelimisha jamii
nzima.
Shule ya Wasichana ya Bunge ilianza
kujengwa Januari 2020 itakamilika Juni mwaka huu na inatarajiwa kuchukua
wanafunzi wa kidato cha tano.
![]() |
Muonekano wa baadhi ya majengo ya shule ya sekondari maalum ya wasichana inayojengwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopo Chamwino, Dodoma. |
Jumamosi, 4 Aprili 2020
Ijumaa, 3 Aprili 2020
Alhamisi, 2 Aprili 2020
MRADI WA KUBORESHA ELIMU YA SEKONDARI (SEQUIP) UTATUMIKA KUBORESHA MAZINGIRA YA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZIA KATIKA SHULE ZA SEKONDARI
Serikali imesema Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 500 ulioidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Dunia hivi karibuni utatumika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za sekondari nchini.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumzia mradi huo ambapo amesema pamoja na kujenga miundombinu ya shule mradi huo utatoa mafunzo kazini kwa walimu na wanafunzi kuhusu masuala ya kidijitali.
Waziri Ndalichako amesema katika kipindi cha miaka minne Serikali katika shughuli za elimu ilijikita zaidi katika kujenga miundombinu kwa sababu mwitikio wa utekelezaji wa Sera ya elimu bila malipo katika ngazi zote za elimu umekuwa mkubwa hivyo mradi huo unakwenda kuongeza miundombinu katika shule za sekondari.
“Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuongeza miundombinu katika maeneo mbalimbali ya elimu baada ya mwitikio mzuri wa elimu bila malipo ambao utaongeza idadi kubwa ya wanafunzi wanaokwenda kujiunga na elimu ya sekondari. Mradi huu utasaidia katika kuboresha na kuongeza miundombinu katika shule za sekondari nchini ambazo zitapokea wanafunzi hao waliotokana na mwitiko wa elimu bila malipo,” amesema Profesa Ndalichako.
Ameongeza kuwa mafunzo kazini yatasaidia kuongeza ujuzi na stadi ambazo zinaendana na wakati wa sasa ili waweze kufundisha vizuri zaidi. Pia mradi huo utatoa mafunzo ya kidijitali kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Aidha, amesema Mradi huo utamuondolea changamoto mtoto wa kike na vikwazo ambavyo vilikuwa vinasababisha asiweze kumaliza elimu yake kwa kuhakikisha inajenga mabweni, shule maalum mpya za wasichana zenye mabweni pamoja na kuimarisha utoaji wa ushauri nasaha ili wanafunzi wanaokuwa na changamoto za kifamilia, kijamii ama mazingira ya shule wawe na mahali pa kusemea ili serikali iweze kuchukua hatua.
“Watoto wa kike wamekuwa wakipata vikwazo kutokana na umbali wa shule na kusababisha kupata changamoto wanapokwenda ama kurudi shuleni kwa hiyo kupitia mradi huu tunakwenda kujenga shule za bweni kwa ajili ya watoto wa kike,” amesisitiza Waziri Ndalichako.
Kuhusu kuondoa changamoto ya wingi wa wanafunzi darasani katika shule za sekondari iliyotokana na elimu bila malipo, Waziri Ndalichako amesema mradi huu utawezesha ujenzi wa shule katika Halmashauri mbalimbali nchini zenye wanafunzi wengi.
Aidha, Waziri Ndalichako amesema mradi huo unakwenda kunufaisha wanafunzi zaidi ya milioni sita na kuongeza kuwa serikali imefungua milango yake katika kupokea ushauri, maoni na mapendekezo kuhusu namna ya utekelezaji wa mradi huo ili kuwezesha kuwa na manufaa kwa nchi.
Jumamosi, 14 Machi 2020
ZIARA YA KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMIIEO

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Peter Serukamba ametoa rai kwa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kutangaza programu na huduma ziazotolewa Chuoni hapo ili wananchi wanufaike na huduma hizo.
Serukamba ametoa rai hiyo Jijini Arusha wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea chuo cha Ufundi Arusha kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa chuoni hapo.

"Nimefurahishwa na ubora wa huduma na wanafunzi wa chuo hiki sasa wakati umefika kwa chuo kujitangaza ili kupata masoko ya bidhaa zinazozalishwa lakini pia kuongeza wanafunzi wengi zaidi kujiunga na kozi zinazofundishwa hapa" amesema Serukamba.
Pia amekitaka Chuo hicho kuanzisha Kampuni itakayosimamia na kufanya kazi mbalimbali kibiashara katika maeneo waliyobobea ikiwemo uhandisi ujenzi, ufundi wa magari, umeme na maeneo mengine, hatua ambayo itasaidia kukuza mapato ya ndani ya Chuo ambayo yatakiwezesha kutekeleza miradi mingine ya kimkakati.

Mheshimiwa Serukamba amesema Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa Miradi ya Serikali ambayo Chuo cha ATC kinasimamia na kukitaka chuo hicho kupanua wigo wa wateja kwa kutafuta miradi toka sekta Binafsi ili kuondoa utegemezi wa Miradi ya Serikali pekee.
Aidha, Mheshimiwa Serukamba ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika wa miundo mbinu ya kufundishia katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na kukipatia kazi za usimamizi wa Miradi ya Ujenzi katika Vyuo vya Ufundi na Ualimu.

Pia amekipongeza Chuo cha Ufundi Arusha kwa kuendesha programmu ya Mafunzo ya muda mfupi ya ufundi ujenzi ambayo mpaka sasa takriban wanafunzi 305 wamehitimu mafunzo hayo, huku akiishauri Wizara ya Elimu, kushirikiniana na Chuo hicho kuhakikisha wahitimu hao wanapata nafasi ya kufanya kazi katika miradi ya ujenzi inayoendelea.

Nae Mbunge wa Biharamulo Magharibi na Mjumbe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Oscar Mukasa amesema kwa mara ya kwanza ameona chuo kimesimama katika dhamira yake, na hivyo kupongeza hatua ya Chuo cha ATC kujikita katika kutoa mafunzo kwa ubora ambayo ndio msingi wa kuanzishwa kwake, akiongeza kuwa vipo vyuo ambavyo vilianzishwa kwa malengo fulani lakini kwa sasa vinatekeleza malengo mengine.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye elimu ya Ufundi kwa kuimarisha vyuo vya ufundi wa kati na ufundi stadi kwani ndiko wataalamu wanapopatikana wa kufanya kazi kwenye viwanda na ndio maana serikali imewekeza takriban sh bilioni 16 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mitambo ya karakana zote za chuo hicho.

“Tangu serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani viwanda 800 vimeanziswa, hii maana yake ni kwamba tunahitaji kuzalisha vijana wengi wenye ujuzi wa kufanya kazi katika viwanda hivyo," amesema Profesa Ndalichako
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ufundi Arusha Prof. Siza Tumbo amesema katika uongozi wake atahakikisha chuo hicho kinajitangaza kwa kupitia njia anuahi za mawasiliano ili huduma zinazotolewa chuoni hapo ziwafikie watanzania wengi zaidi, ikiwa ni pamoja na kuwa na mkakati wa kuongeza idadi ya wasichana kujiunga na chuo hicho.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha Dkt Musa Chacha amesema kwa sasa Chuo kina mipango mingi ikiwa ni pamoja na kujenga bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 500, kuongeza mapato ya ndani kutumia kazi zinazofanyika, kuendeleza kituo cha mafunzo ya nishati jadidifu cha Kikuletwa na kituo cha mafunzo ya kilimo na umwagiliaji cha Oljoro pamoja na ukarabati wa miundombinu ya Chuo.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii iko Mkoani Arusha katika ziara ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa katika Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)