Alhamisi, 15 Februari 2018

Waziri Ndalichako :Maafisa Elimu Nchini fuateni Sera na Miongozo inayotolewa na Wizara


Maafisa Elimu nchini wametakiwa kufuata miongozo na sera inayotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa kutekeleza majukumu yao na endapo watakiuka maelekezo hayo wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa Wilayani Muleba mkoani Kagera na kusema kuwa kumekuwa na tabia kwa baadhi ya  Maafisa Elimu kupeleka wanafunzi wengi kwenye shule kuliko uwezo wa shule.

Waziri Ndalichako amesema kuwa hali hiyo inachangia kuwepo kwa matokeo mabaya  na hivyo amewaagiza wathibiti ubora wa shule nchini kukagua shule zote ili kuondoa changamoto hizo.

Katika ziara hiyo Waziri Ndalichako pia ametembelea na kukagua shule ya Sekondari ya Profesa Joyce Ndalichako iliyoko Wilayani Muleba ambapo amewaagiza walimu wa shule hiyo kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo wanafanya vizuri kitaaluma.

" Walimu hii shule imebeba jina langu, nawaomba sana matokeo ya shule hii yaendane na Mimi mwenyewe kwa maana ya wanafunzi kufanya vizuri na Wizara itahakikisha inazipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zilizopo katika shule hii," alisema Waziri Ndalichako.

Katika ziara hiyo Waziri Ndalichako alitembelea na kukagua Chuo cha Ualimu katoke, shule ya Sekondari Anna Tibaijuka zilizopo Wilayani Muleba.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni