Ijumaa, 14 Desemba 2018

OLE NASHA ASEMA KUSTAAFU SIYO ADHABU NI MAFANIKIO


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ameitaka Wizara hiyo kuweka mkakati endelevu wa kutoa mafunzo kwa watumishi kuhusu masuala ya kustaafu na sio kusubiria kutoa mafunzo hayo wakati mtumishi anakaribia kustaafu.

Mhe. Ole Nasha ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo kwa watumishi wa Wizara hiyo wanaotarajia kustaafu ambapo amesema kustaafu ni mchakato ambao unaanza pale mtumishi anapoajiriwa hadi anapofikia umri wa kustaafu.

“Idara ya Utawala na Rasilimali watu mnapaswa kutambua kustaafu ni mchakato unaoanza tangu mtumishi anapoajiriwa.  Kama unataka kumtayarisha mtumishi aweze kustaafu vizuri au kumpa maarifa ya kumwezesha kuishi vizuri baada ya kustaafu unapaswa kuanza mapema na sio kusubiri kutoa mafunzo wakati mtumishi amebakiza mwaka mmoja au miezi sita kustaafu,”  alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa mafunzo ya kustaafu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara hiyo ili kuwapatia maarifa ya ubunifu na uendeshaji wa miradi ya uzalishaji mali baada ya kustaafu.

Ole Nasha ameitaka Idara ya Utawala ya Wizara hiyo kuhakikisha inaweka kumbukumbu za watumishi vizuri na kwa usahihi ili kuepuka ucheleweshaji wa mafao unaosababishwa na kutotunza kumbukumbu za watumishi hao ipasavyo.

Naibu Waziri huyo pia amewataka watumishi kuelewa kuwa kustaafu siyo adhabu ni mafanikio hivyo wanapaswa kujitambua na kutumia taaluma waliyo nayo na maarifa waliyoyapata katika mafunzo kuendeleza maisha yao baada ya kustaafu.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya watumishi wanaotarajia kustaafu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mafunzo hayo yamefanyika Jijini Dodoma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Gaudencia Mmasi amesema mafunzo hayo yamehusisha watumishi wanaotarajia kustaafu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na wale walio kwenye Vyuo Vya Ualimu, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na Ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule.

Akizungumza kwa niaba ya Washiriki wa Mafunzo hayo. Katibu wa washiriki wa mafunzo ya kustaafu, Peter Kyabwazi aliiomba Wizara kuyafanya mafunzo hayo kuwa endelevu ili kuwasaidia wastaafu.

Mafunzo hayo kwa watumishi ambao wanatarajiwa kustaafu yamefanyika kwa siku tano kuanzia Desemba 10 na kuhitimishwa leo.
Washiriki wa mafunzo ya kustaafu wakifuatlia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa kufunga mafunzo kwa watumishi wa Wizara hiyo wanaotarajia kustaafu.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tz




Chuo cha Masomo ya Biashara
na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S.L.P. 10,
40479 DODOMA.

Tarehe: 14 Desemba, 2018.


WARAKA NA. 1 WA MWAKA 2018
MWONGOZO WA UUNDAJI NA UENDESHAJI WA KAMATI NA BODI ZA SHULE
Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu Na. 25 ya mwaka 1978 na Rekebisho lake Sura 353 ya mwaka 2002 kila Shule ya Msingi na Sekondari sharti iwe na Kamati ya Shule (kwa shule za Awali na Msingi) au Bodi ya Shule (kwa shule za Sekondari) iliyo hai. Aidha, Serikali imekuwa ikitoa miongozo juu ya utaratibu wa kuunda na kuendesha Kamati na Bodi hizo.
Waraka huu unalenga kutoa mwongozo mahsusi kuhusu muundo, wajibu na uendeshaji wa Kamati na Bodi za shule.

1.0        KAMATI ZA SHULE ZA AWALI NA MSINGI/BODI ZA SHULE ZA SEKONDARI
1.1     Kamati za Shule za Awali na Msingi za Serikali na Zisizo za Serikali
Shule zote zitakuwa na Kamati (Kwa Shule za Awali na Msingi) na Bodi kwa Shule za Sekondari).

1.2   Sifa za Wajumbe na Utaratibu wa Uundaji wa Kamati na Bodi za Shule
a)            Itaundwa na wajumbe wasiopungua tisa (9),
b)            Diwani, Mwenyekiti na Katibu wa Serikali ya Kijiji/Mtaa (wa eneo shule ilipo) hawatakuwa na sifa ya kuwa wajumbe wa Kamati/Bodi ya shule. Hii ni kuepusha mgongano wa kiutendaji kutokana na jukumu lao la kuiwakilisha Serikali katika ngazi zao za utawala,
c)            Kamati itakuwa na vikao visivyopungua viwili (2) kwa mwaka. Mwenyekiti anaweza kuitisha kikao cha dharura kama kuna suala linalohitaji kujadiliwa,
d)            Wajumbe wa Kamati/ Bodi wanatakiwa wawe na sifa zifuatazo:
                                                  i.Wawe na elimu ya Kidato cha Nne au zaidi,
                                                ii.Wawe na shughuli halali za kujipatia kipato,
                                              iii.Uwiano wa wajumbe uzingatie jinsi zote mbili,
                                              iv.Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti achaguliwe na Wajumbe wa Kamati kutoka miongoni mwao.
e)            Kamati ya Shule itakuwa na kamati ndogondogo tatu (3) zifuatazo:
                                                i.     Kamati ya Taaluma, Malezi na Unasihi,
                                                ii.Kamati ya Fedha, Mipango na Miundombinu, na
                                              iii.Kamati ya Mazingira, Afya na Chakula.
f)              Wajumbe wa Kamati/Bodi za Shule watathibitishwa na Afisa Elimu wa Wilaya.


1.3 Wajibu na Majukumu ya Kamati ya Shule
a)            Kuandaa/kuidhinisha Mpango wa Maendeleo ya shule na mikakati ya utekelezaji wake,
b)            Kuitisha na kuendesha vikao vya wazazi na kutoa taarifa ya maendeleo ya shule,
c)            Kwa shule za serikali kuidhinisha matumizi ya fedha za shule na kusimamia matumizi bora ya fedha za uendeshaji na maendeleo ya shule,
d)            Kwa shule zisizo za serikali, kushauri namna bora ya matumizi ya fedha  kwa miradi ya maendeleo ya shule ikiwemo ukarabati wa miundombinu,
e)            Kuhimiza ujenzi wa shule na usafi wa mazingira ya shule na wanafunzi,
f)             Kwa shule za serikali, kusimamia ujenzi na ukarabati wa madarasa na miundombinu mingine na utunzaji wa mazingira ya shule,
g)            Kusimamia ufundishaji na ujifunzaji shuleni kwa kuhakikisha kuwa walimu wanafanya kazi zao kwa ufanisi,
h)            Kuhakikisha wanafunzi wote wanahudhuria masomo kwa mujibu wa sheria,
i)             Kuhakikisha shule inakuwa na Sanduku la Huduma ya Kwanza na pia shule inadumisha elimu ya afya shuleni kwa njia mbalimbali,
j)             Kuhakikisha huduma za Malezi na Unasihi kwa wanafunzi zinaendeshwa kwa ufanisi shuleni,
k)            Kutathmini uhalali wa kumsimamisha/kumfukuza shule mwanafunzi bila upendeleo wala kushawishiwa na mtu au kikundi chochote kabla ya kuhalalisha uamuzi huo,
l)             Kuhakikisha Kamati inakutana ndani ya wiki mbili inapotokea shule imependekeza kumsimamisha/kumfukuza mwanafunzi ili uamuzi sahihi utolewe kwa wakati kuepusha ucheleweshaji unaoweza kuathiri haki za kielimu za mwanafunzi husika pasipo sababu za msingi, na
m)         Kamati itafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu (3).


2.0 MUUNDO WA KAMATI/BODI ZA SHULE
Katika kuunda Kamati na Bodi za Shule za Serikali na zisizo za Serikali mambo yafuatayo yatazingatiwa:

2.1   Wajumbe wa Kamati za Shule za Awali na Msingi za Serikali
                           i.            Mwalimu Mkuu ambaye pia atakuwa Katibu wa Kamati,
                        ii.            Mwalimu wa Taaluma katika shule,
                      iii.            Wawakilishi wawili (2) wa walimu shuleni,
                       iv.            Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mkuu wa Kitengo naye atakua Mjumbe,
                         v.            Wajumbe watatu (3) watakaochaguliwa na mkutano wa wazazi, na
                       vi.            Mkazi jirani atakayeteuliwa na Mkuu wa shule.

2.2     Kamati za Shule za Awali na Msingi Zisizo za Serikali
                             i.         Mkuu wa shule ambaye atakuwa Katibu wa Kamati ya shule,
                           ii.         Mmiliki wa shule,
                         iii.         Mwalimu wa Taaluma,
                         iv.         Wajumbe watatu (3) watakaoteuliwa na Mmiliki wa Shule,
                           v.         Mwakilishi mmoja (1) wa walimu shuleni.  
                         vi.         Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mkuu wa Kitengo naye atakua Mjumbe,
                    vii.            Mzazi mmoja (1) anayewakilisha wazazi wenye watoto katika shule hiyo atakayechaguliwa na Mkutano Mkuu wa Wazazi,
                  viii.            Mkazi mmoja jirani atakayeteuliwa na Mwenye shule.

2.3   Bodi za Shule za Sekondari za Serikali
                              i.         Mkuu wa Shule ambaye atakuwa Katibu wa Bodi,
                           ii.         Mwalimu wa Taaluma katika shule,
                         iii.         Wawakilishi wawili (2) wa walimu shuleni,
                          iv.         Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum; Mkuu wa Kitengo pia atakua mjumbe katika Bodi ya shule,
                            v.         Wajumbe watatu (3) wanaowakilisha wazazi wenye watoto katika shule hiyo watakaochaguliwa na Mkutano Mkuu wa wazazi, na
                          vi.         Mkazi jirani atakayeteuliwa na Mkuu wa shule.

2.4   Bodi za Shule za Sekondari Zisizo za Serikali
                    i.              Mkuu wa shule ambaye atakuwa Katibu wa Bodi ya shule,
                  ii.              Mmiliki wa shule,
                iii.              Mwalimu wa Taaluma,
                iv.              Wajumbe watatu (3) watakaoteuliwa na Mmiliki wa Shule,
                  v.              Mwakilishi mmoja (1) wa walimu shuleni.  
                vi.              Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mkuu wa Kitengo pia atakua Mjumbe,
              vii.              Mzazi mmoja (1) anayewakilisha wazazi wenye watoto katika shule hiyo atakayechaguliwa na Mkutano Mkuu wa Wazazi,
            viii.              Mkazi mmoja jirani atakayeteuliwa na Mwenye Shule.

Waraka huu unafuta Nyaraka zote za awali zilizokuwa zinatoa Mwongozo kuhusu Kamati za Shule za Awali na Msingi na Bodi za Shule za Sekondari na utaanza kutumika kuanzia Januari, 2019.




Dkt. Edicome C. Shirima

KAIMU KAMISHNA WA ELIMU



Nakala:      Makatibu Tawala wa Mikoa,
                    Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya/Mji/Manispaa/Jiji,
                    Wathibiti Ubora wa Shule Wakuu Kanda na Wilaya.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tz



Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S.L.P. 10,
40479 DODOMA.

Tarehe: 10 Desemba, 2018.

WARAKA WA ELIMU NA. 2 WA MWAKA 2018
UTARATIBU WA KUKARIRI DARASA KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI

Serikali imekuwa na utaratibu wa kupokea na kushughulikia maombi ya kukariri darasa kutoka kwa baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wanaoshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali. Aidha, Shule Zisizo za Serikali zimekuwa zikiwakaririsha darasa wanafunzi wanaoshindwa kufikia viwango vya ufaulu vinavyopangwa na shule husika.

Kufuatia hali hiyo kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wazazi na walezi kutokana na kutoshirikishwa ipasavyo katika kufanya uamuzi wa mwanafunzi kukariri darasa. Kutokana na changamoto zinazojitokeza kwenye suala hili wizara inapenda kutoa maelekezo kama ifuatavyo:

1.0 Kukariri Darasa
Maombi ya Kukariri darasa kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari yatashughulikiwa kama ifuatavyo:
(a)                  Maombi ya Kukariri darasa la I, II na III yatashughulikiwa na Halmashauri husika ambapo darasa la IV, V na VI kwa Shule za Msingi na kidato cha 1, 2, 3, na 5 kwa shule za Sekondari yatashughulikiwa na Mkoa;
(b)         Maombi ya kukariri darasa la VII kwa shule za Msingi na Kidato cha 4 na 6 ambayo ni madarasa ya mitihani ya mwisho ya Kitaifa yataendelea kutumwa kwa Kamishna wa Elimu ili kupata kibali cha kukariri; na
(c)                  Mwanafunzi atakayeomba na kukubaliwa kukariri katika ngazi ya Elimu ya Msingi na Sekondari atapewa fursa ya kukariri mara moja. Endapo mamlaka inayohusika itaona umuhimu wa Mwanafunzi kukariri darasa  mara ya pili, ataweza kupewa fursa hiyo.

(d)         Utaratibu wa Maombi ya Kukariri Darasa
                                 i.        Mzazi wa mwanafunzi wa darasa la I, II na III anatakiwa kuandika barua ya maombi ya kukariri darasa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika;
                               ii.       Mzazi wa mwanafunzi wa  darasa la IV, V na VI kwa shule za Msingi na Kidato cha 1, 2, 3, na 5 kwa shule za Sekondari anatakiwa kuandika barua kwa Katibu Tawala wa Mkoa;
                        iii.            Mzazi wa mwanafunzi wa darasa la VII kwa Shule za Msingi na Kidato cha 4 na 6 kwa shule za Sekondari anatakiwa kuandika barua kwa Kamishna wa Elimu kulingana na darasa husika;
                        iv.            Maombi yote yapitie kwa Mkuu wa Shule anayosoma mwanafunzi na Mkurugenzi wa Halmashauri husika, na
                           v.            Kila barua ya maombi ni lazima iwe na viambatisho vifuatavyo:
a.      Picha 2 za mwanafunzi aina ya pasipoti;
b.     Namba ya kuandikishwa shuleni; na
c.      Nyaraka zozote muhimu kulingana na sababu ya maombi                                        yanayowasilishwa.

2.0    Kukariri Darasa Wanafunzi Wanaoshindwa Kufikia Viwango vya Ufaulu Vilivyowekwa na Shule

Wizara inakumbusha kuwa wanafunzi waliofaulu mitihani ya upimaji inayofanywa kitaifa (Darasa la IV na Kidato cha 2) wanakuwa na sifa ya kumaliza ngazi ya elimu husika bila kukariri.

Hata hivyo, kwa makubaliano ya maandishi kati ya mzazi au mlezi na Mkuu wa shule ya Serikali au isiyo ya Serikali, mwanafunzi ataruhusiwa kukariri Darasa kwa kufuata utaratibu ulioainishwa hapo juu ambapo mzazi atakuwa ameridhia.

Waraka huu unafuta nyaraka zote zilizotangulia zilizokuwa zikitoa maelekezo kuhusu utaratibu wa kukariri darasa na utaanza kutumika Januari, 2019.



Dkt. Edicome C. Shirima
KAIMU KAMISHNA WA ELIMU