Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ameitaka Wizara hiyo kuweka mkakati endelevu
wa kutoa mafunzo kwa watumishi kuhusu masuala ya kustaafu na sio kusubiria
kutoa mafunzo hayo wakati mtumishi anakaribia kustaafu.
Mhe. Ole Nasha ametoa agizo hilo jijini
Dodoma wakati akifunga mafunzo kwa watumishi wa Wizara hiyo wanaotarajia kustaafu
ambapo amesema kustaafu ni mchakato ambao unaanza pale mtumishi anapoajiriwa hadi
anapofikia umri wa kustaafu.
“Idara ya Utawala na Rasilimali watu
mnapaswa kutambua kustaafu ni mchakato unaoanza tangu mtumishi anapoajiriwa. Kama unataka kumtayarisha mtumishi aweze kustaafu
vizuri au kumpa maarifa ya kumwezesha kuishi vizuri baada ya kustaafu unapaswa kuanza
mapema na sio kusubiri kutoa mafunzo wakati mtumishi amebakiza mwaka mmoja au miezi
sita kustaafu,” alisisitiza Naibu Waziri
Ole Nasha.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akimkabidhi cheti
mmoja wa washiriki wa mafunzo ya kustaafu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara hiyo ili kuwapatia maarifa ya
ubunifu na uendeshaji wa miradi ya uzalishaji mali baada ya kustaafu.
Ole Nasha ameitaka Idara ya Utawala
ya Wizara hiyo kuhakikisha inaweka kumbukumbu za watumishi vizuri na kwa usahihi
ili kuepuka ucheleweshaji wa mafao unaosababishwa na kutotunza kumbukumbu za watumishi
hao ipasavyo.
Naibu Waziri huyo pia amewataka watumishi
kuelewa kuwa kustaafu siyo adhabu ni mafanikio hivyo wanapaswa kujitambua na kutumia
taaluma waliyo nayo na maarifa waliyoyapata katika mafunzo kuendeleza maisha
yao baada ya kustaafu.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza wakati wa
kufunga mafunzo ya watumishi wanaotarajia kustaafu wa Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia. Mafunzo hayo yamefanyika Jijini Dodoma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi
wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Gaudencia Mmasi amesema mafunzo hayo yamehusisha
watumishi wanaotarajia kustaafu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na
wale walio kwenye Vyuo Vya Ualimu, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na Ofisi za Uthibiti
Ubora wa Shule.
Akizungumza kwa niaba ya Washiriki
wa Mafunzo hayo. Katibu wa washiriki wa mafunzo ya kustaafu, Peter Kyabwazi aliiomba
Wizara kuyafanya mafunzo hayo kuwa endelevu ili kuwasaidia wastaafu.
Mafunzo hayo kwa watumishi ambao wanatarajiwa
kustaafu yamefanyika kwa siku tano kuanzia Desemba 10 na kuhitimishwa leo.
Washiriki
wa mafunzo ya kustaafu wakifuatlia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha wakati wa kufunga mafunzo kwa watumishi wa Wizara
hiyo wanaotarajia kustaafu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.