Alhamisi, 9 Agosti 2018

WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA KUSIMAMISHWA KAZI MAAFISA WATATU WA WIZARA YA ELIMU.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Joyce  Ndalichako  amemuagiza  Katibu  Mkuu wa Wizara hiyo  Dk. Leonard Akwilapo kumsimamisha kazi Afisa manunuzi  Audifasy Myonga na watumishi wengine wawil wa Chuo cha Ualimu Morogoro.

Waziri Ndalichako ametoa maagizo hayo mkoani Morogoro baada ya kutembelea chuo Cha Ualimu Morogoro  na kukuta idadi kubwa ya vifaa vya maabara visivyotumika huku muda wa matumizi ya vifaa hivyo  ukikaribia kuisha muda wake wa matumizi.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua baadhi ya vifaa vya maabara katika Chuo cha Ualimu Morogoro kilichopo mkoani Morogoro ambapo amekuta vifaa na madawa ya maabara ambayo yamehifadhiwa bila kutumika tangu mwaka 2016.
Ndalichako amesema ununuzi wa vifaa hivyo unaonyesha kuwa na shaka kwani vifaa hivyo vilinunuliwa kwa awamu mbili ndani ya mwezi mmoja huku gharama ya manunuzi ikionyesha kupanda mara mbili hadi tatu kutoka gharama ya awali.

“Mkuu wa Chuo ameeleza vizuri kabisa kuwa vifaa hivyo vilinunuliwa bila wao kushirikishwa, sasa unajiuliza mnunuzi amewezeje kununua vifaa vya maabara bila kuwashirikisha watumiaji,” alihoji Waziri Ndalichako .
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na watumishi wa Chuo cha Ualimu Morogoro kilichopo mkoani Morogoro. Waziri pia alisikiliza changamoy=to walizonazo watumishi hao. 

Pia, Waziri Ndalichako  ametembelea shule ya Sekondari ya Mzumbe kwa lengo la kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo unaofanywa na wizara ambapo amewataka walimu na wanafunzi kuhakikisha wanafanya vizuri katika masomo yao ili wafaulu kwa viwango vya juu.



Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na Naibu Katibu Mkuu Dk. Avemaria Semakafu wakikagua baadhi ya miundombinu iliyokarabatiwa katika shule ya Sekondari Mzumbe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni