Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dkt.
Shukuru Kawambwa amewataka wazazi kusimamia ipasavyo maadili ya watoto
wao ili waweze kufanikiwa na kufikia malengo
waliyojiwekea kitaaluma.
Pia aliwataka kushirikiana na walimu katika kuhakikisha watoto wanakuwa na
nidhamu ya kuridhirisha katika jamii inayowazunguka.
Dkt
Kawambwa alitoa wito huo katika mahafari ya kuwatunuku vyeti wanafunzi wa darasa
la saba katika shule ya Msingi Kongo
iliyopo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani. Ambapo aliwataka walimu na wazazi
kuhakikisha wanawasisitiza wanafunzi kutii sheria za shule kama vile uvaaji wa sare sahihi ya shule,
kuheshimiana na utumiaji wa lugha nzuri.
“Wazazi
tuna jukumu kubwa la kusimamia suala la maadili ya watoto wetu. Hili ni suala ambalo huwezi
kulitenanisha na mafanikio bora kitaaluma. Mara nyingi mtoto wenye nidhamu na
maadili mema daima hufanya vizuri darasani na yule asiye na nidhamu huporomoka
katika taaluma. Nasisitiza nidhamu na taaluma huenda pamoja, haiwezekani
kuvitenganisha hata mara moja.” Alisisitizi Dkt. Kawambwa.
Aidha, aliwataka wanafunzi wote nchini wanaomaliza darasa
la saba kujiandaa vyema kufanya Mitihani yao inayotarajiwa kuanza, kujitahidi kutulia na kutumia vyema maarifa
yote waliyopata kutoka kwa walimu wao. Aliwakumbusha kwamba watakapomaliza
mitihani yao wasijisahau na kufikiri kuwa sasa elimu ndio basi bali watambue
kuwa safari ya kutafuta elimu ndio inaanza.
Dkt Kawambwa aliwataka kutenga muda wa kujiandaa kwa
masomo ya sekondari mara wanapomaliza mitihani yao ya darasa la saba. "Nawasihi
muwe raia wema wenye kuwajibika katika jamii yote. Maisha sio lele mama! wekeni
juhudi katika masomo, elimu ndio msingi bora wa maisha, msidanganyike hakuna
njia ya mkato katika kufanikiwa katika maisha". aliongeza Dkt.
Kawambwa.
Waziri Kawambwa aliwataka walimu wote nchini kutambua
kuwa shughuli za kila siku shuleni zinahitaji juhudi za hali ya juu. Aliwataka kuboresha
zaidi utendaji kazi wao ili kufikia matarajio ya Taifa ya kuwa na watu walioelimika na wenye uwezo wa
kuhimili changamoto zinazotokana na
mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
Waziri aliwasisitiza walimu kukabiliana na changamoto
zinzojitokeza katika sekta ya elimu kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea, badala
yake kuhakikisha wanapanga mipango yao, wanajiwekea malengo ya muda mfupi na
mrefu na kubuni mikakati sahihi inayotekelezeka ambayo itawezesha kufikia
malengo waliyojiwekea.
Aidha, aliwashauri
wazazi kutoa ushirikiano wa hali ya juu
katika suala zima la kufanikisha matokeo mazuri ya ufaulu kuanzia madarasa ya
awali, la kwanza hadi darasa la Saba. "Yote haya yanawezekana pale
tutakapotekeleza wajibu wetu wa kusimamia vyema yale yote wanayofundishwa
watoto wetu wanapokuwa shuleni. Watoto hupewa mazoezi mbalimbali (homework) na walimu
wao ili wazifanye wanapokuwa nyumbani, ni jambo la msingi tukitenga muda
kusimamia katika eneo hili. "
Pia aliwataka
wazazi kuhakikisha wanatimiza jukumu lao la kuwapatia watoto mahitaji muhimu
yanayotakiwa shuleni. Kwani mara nyingi
utoro wa Wanafunzi shuleni huchangiwa sana wanafunzi wanapo shindwa kupatiwa
mahitaji yao ya shule.
Aliwataka wanafunzi wanaobaki shuleni kujitahadi kuzingatia Masomo. Kwani kipindi walichonacho
shuleni ni kifupi sana, lakini ni kipindi
muhimu sana katika kuandaa maisha yao ya baadaye. Amewataka kuwasikivu,
kutii sheria za shule, tekeleza majukumu yao wanayopewa katika masomo, kuepuka
vitendo viovu katika jamii. Alwasihi kuwa na nidhamu inayopendeza machoni na
mioyoni mwa wazazi, walezi na walimu wao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.