Ijumaa, 14 Novemba 2014

Wakaguzi wa Shule watakiwa kusimamia ubora wa Elimu nchini

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Consolata Mgima ameitaka idara ya Ukaguzi wa Shule kusimamia ubora wa Elimu nchini, kwa kuhakikisha kuwa sera, sheria, kanuni na viwango vya elimu vilivyowekwa katika mfumo wa utoaji elimu vinazingatiwa ipasavyo kwa kuhakikisha mitaala na viwango vya elimu vilivyowekwa vinafuatwa ili kuongeza ufanisi na ubora katika elimu. 
Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa Elimu uliofanyika mjini Morogoro hivi karibu uliokuwa ukijadili kuhusu umuhimu wa uanzishwaji wa mfumo wa Menegement ya  Habari na Mawasiliano katika Idara ya  Ukaguzi wa Shule unaotekelezwa kwa kusirikiana kati ya Wizara ya Elimu  na Mafunzo ya Ufundi na Shirika linalohudumia Watoto Duniani UNICEF, alisema Kwa kutambua hilo, wizara imekuwa ikiiwezesha ukaguzi wa shule kwa kuongeza wakaguzi wa shule, vitendea kazi na kuongeza vyombo vya usafiri.
Naibu Katibu Mkuu alisema Uanzishwaji wa mfumo wa Menejimenti ya Habari na Mawasiliano wa Idara ya Ukaguzi wa Shule, unategemewa kuwa utaleta mafanikio makubwa katika upatikanaji wa yale yaliyojiri baada ya shule kukaguliwa.  Mafanikio hayo yatawezesha wadau wengi kupata taarifa za ukaguzi kuliko ilivyo hivi sasa. 
“Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa suala la ubora wa elimu ni la ushirikishwaji wa wadau wote katika ngazi zote ikiwemo jamii hivyo naipongeza idara ya ukaguzi wa shule pamoja na UNICEF kwa mkakati waliokuja nao wa kuanzisha vituo vya mafunzo vya jamii katika kata, kwa uhakika jamii ikishirikishwa  katika hatua  za awali  elimu itaimarika.” Alisisitiza Naibu Katibu Mkuu 
Akizungumzia Mfumo huo Kaimu Mkurugenzi wa idara ya Ukaguzi wa shule Dkt. Edicome Shirima alisema utekelezaji wa mfumo ulianza Augusti 2011 ukitekelezwa katika kata 35 zilizo katika wilaya 7 za majaribio (Pilot). Wilaya hizo ni Bagamoyo, Hai, Makete, Magu, Siha Temeke na Mtwara Vijijini.
“Lengo ni kuweka taarifa za Ukaguzi wa shule katika  kanzidata (data base) itakayoonesha shule na ubora wake (School -Level Quality Assurance Data)”. Alielezea Dkt. Shirima
Taarifa hizo zilizomo katika mfumo huo zinaweza  kuonwa na wadau wote wanaohitaji  kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Aidha zitasaidia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  kutoa maamuzi mbalimbali yanayohusu  elimu. Baada ya kukamilika kwa  uandaaji wa mfumo wa (IMIS) utaingizwa katika Mtandao mkubwa wa   Elimu Kisekta (ESMIS)
Akifafanua jinsi data hizo zinavyokusanywa Dkt shirima alifafanua kuwa Katika  maandalizi ya IMIS,  orodha hakiki inayotumika Katika ukaguzi wa shule wa jumla huchambuliwa kwa ufasaha na  kuwekwa katika  mtirirIko mzuri utakaowezesha data zitakazokuwa zimekusanywa kupitia vyanzo mbalimbali  kama vile  sensa ya uandikishaji kwa darasa la  awali na darasa la kwanza  na  hatua za Ufundishaji (lesson observation) kupatikana na kutumika  Katika  uandikishaji na kuboresha ufundishaji. Haya yote yamefanyika kwa kuzingatia viwango vya msingi vya elimu (Basic Standard)
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukaguzi Dkt. Shirima alisema zana  za kukusanyia taarifa imendaliwa Katika mifumo miwili ambayo ni Fomat A kwajili ya  msimamizi wa shule  na Fomati B kwa ajili ya  mkaguzi wa shule, ambayo  itaonesha  pia    hatua za Ufundishaji  darasani (lesson observation)
Orodha hakiki zote zitaonesha  kipengere  kinachohitaji marekebisho Katika utendaji
Walengwa wa Uanzishaji wa Mfumo wa Habari na Mawasiliano  umewalenga Waratibu Elimu Kata na Wakaguzi wa Shule kwa kuwa  ni wadau muhimu  Katika usimamizi wa elimu,   hivyo  wamepewa jukumu kubwa Katika kusimamia na kuhakikisha ubora wa  elimu unapatikana.
“Mratibu Elimu wa Kata kama msimamizi wa shule aliye karibu na shule akisaidiana na mwalimu mkuu ambaye ni msimamizi wa shule wa ndani.  Kwa pamoja   wana nafasi kubwa sana katika kusimamia elimu Katika maeneo yao. Kwani wataweza kutayarisha taarifa na kuzitoa kwa wadau  kwa wakati, vilevile zitawasaidia wakaguzi wa shule kufahamu mahali gani panahitaji  marekebisho au kutiliwa mkazo.” Alisisitiza Dkt. Shirima
Lengo linguine la Mfumo huu ni kuzifanya jamii zinazoizunguka shule kutambua kuwa shule ni sehemu yake na hivyo kuhusika moja kwa moja katika katika kufuatilia maendeleo ya shule. Ili kuhakikisha kuwa jamii   inashirikishwa kikamilifu.

“Ili kufikia lengo la kushirikisha jamii vimeanzishwa vituo vya mafunzo ngazi ya kata “Community Learning Centers (CLC)”.  Katika vituo hivyo, jamii inapata nafasi  kusoma taarifa za shule,  kutoa maoni  na kurekebisha mapungufu yaliyo ndani ya uwezo wao. Fursa hii itaongeza uwajibikaji wa menejimenti na   kamati  za shule  kwa jamii.” Alifafanua Dkt. Shirima 

 



















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.