Jumapili, 27 Septemba 2020

KAMUSI YA KWANZA YA LUGHA YA ALAMA YA KIDIJITALI YAZINDULIWA

 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua Kamusi ya kwanza ya lugha ya alama ya kidijitali yenye lengo la kupunguza changamoto ya mawasiliano katika ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi viziwi. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akizungumza wakati wa  uzinduzi wa Kamusi ya kwanza ya Lugha ya Alama ya kidijitali ya Tanzania na Mwongozo wa Utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Sekondari kwa wanafunzi viziwi wakati wa kikele cha maadhimisho ya viziwi yaliyofanyika Mkoani Tabora

Akizindua kamusi hiyo Mkoani Tabora, katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi yenye kauli mbiu “Kuhakikisha upatikanaji wa haki za binadamu kwa Viziwi”, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Ave Maria Semakafu amesema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi yote yenye ulemavu kupata elimu na huduma nyingine za kijamii. 

Dkt Semakafu amesema pamoja na maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu, kundi la viziwi lilikuwa limeachwa nyuma huku changamoto kubwa ikiwa ni mawasiliano na kutokuwepo kwa walimu wa kutosha hasa katika ngazi ya sekondari ndio maana imeandaa kamusi hiyo kuwe na lugha moja ya alama na kutoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha katika shule zinazopokea watoto viziwi. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akizindua Kamusi ya kwanza ya Lugha ya Alama ya kidijitali ya Tanzania na Mwongozo wa Utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Sekondari kwa wanafunzi viziwi wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi  yaliyofanyika Mkoani Tabora

“Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na lugha moja ya alama kwa ajili ya kuwezesha mawasiliano ya watumiaji wa lugha hiyo, hivyo itaendelea kusimamia uendelezaji na usanifishaji wa lugha ya alama ili kuwezesha utoaji elimu, kurahisisha ujifunzaji na kuboresha mawasiliano katika jamii.,”alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Nae Kamisha wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi duniani ndio mwanzo wa mafanikio katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji nchini kwani ni siku ambayo kamusi ya lugha ya alama ya kwanza nchini tena ya kidijitali inazinduliwa pamoja na mwongozo wa utekelezaji wa mtaala wa elimu ya sekondari kwa wanafunzi viziwi.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akionesha kishkwambi chenye kamusi huku Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Magret Komba akionesha Mwongozo wa Utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Sekondari kwa wanafunzi viziwi mara baada ya kuzinduliwa katika kilele cha maadhimisho ya viziwi yaliuofanyika Mkoani Tabora

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania(TET)Dkt. Aneth Komba  anasema Taasisi anayoisimamia ndio walipewa jukumu la kuandaa Kamusi hiyo  na kwamba imeandaliwa kwa kufata taratibu zote ikishirikisha wadau wote na kwamba itatumiwa na wanafunzi viziwi kutoka Tanzania Bara na Visiwani. 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi viziwi walioshika vishkwambi vyenye Kamusi ya Lugha ya Alama mara  baada ya kuzindua kamusi hiyo katika kilele cha maadhimisho viziwi yaliyofanyika  Mkoani Tabora

Mkurugenzi wa Kitengo cha Elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Magret Matonya amesema uzinduzi wa Kamusi hiyo ni muendelezo wa jitihada za Serikali kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini wakiwemo viziwi wanapata elimu bora. Aidha ameongeza kuwa  Wizara imeanza ujenzi wa shule ya mfano ya viziwi  katika Halmashauri ya Masasi Mkoani Mtwara ikiwa ni jitihada za kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji wanafunzi viziwi ambapo ujenzi wake utagharimu bilioni 1.5.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Taifa (CHAVITA) Selina Mlemba amesema wanaishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kwamba wanaamini miaka michache ijayo watapata wataalamu wengi katika maeneo mbalimbali wakiwemo madaktari kwa kuwa sasa wamepata kamusi itakayowawezesha kusoma bila changamoto.

Mtaalamu elekezi wa uandaaji wa Kamusi ya lugha ya alama kutoka Archbishop Mihayo University College (AMUCTA) Profesa Henry Muzale amasema uaandaji wa kamusi hiyo umezingatia changamto zote za viziwi na hii ni kutokana na utafiti uliofanyika katika shule zenye watoto viziwi ikiwemo Njombe viziwi ambao  ufaulu wao uliendelea kushuka.

Wadau, wanachama wa Chama cha Viziwi Taifa wakiwa kwenye maandamano wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya viziwi iliuofanyika Mkoani Tabora

Kilele cha maadhimisho ya wiki ya Viziwi duniani kitaifa yamefanyika mkaoni Tabora ikiwa ni hatua ya kuenzi historia ya chimbuko la elimu kwa viziwi kwani shule ya kwanza ya viziwi nchini Tanzania ilianzishwa katika mkoa huo katika shule ambapo maadhimisho yamefanyika.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni