Ijumaa, 29 Novemba 2019

NDALICHAKO AZINDUA CHUO CHA VETA NDOLAGE WILAYANI MULEBA - 380 KUDAHILIWA JANUARI 2020

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezindua chuo kipya cha VETA Ndolage kilichopo Kamachumu Wilaya ya Muleba mkoani Kagera kilichojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 281.

Ujenzi wa Chuo hicho ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kushirikiana na jamii kufikisha Elimu ya Ufundi karibu na Wananchi pamoja na kujenga Vyuo vya VETA katika kila Wilaya nchini ifikapo mwaka 2020, ambapo Wizara imetenga zaidi ya Sh. bilioni 40 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 25 nchini.

Ujenzi wa Chuo cha Ndolage ulianzishwa na Wananchi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Muleba  Kaskazini, Charles Mwijage ambapo wananchi walitoa kiwanja na kuanza ujenzi wa madarasa kwa kutumia michango yao.

Akizungumza katika hafla hiyo Profesa Ndalichako amewataka VETA  kuhakikisha wanajenga majengo yote yanayohitajika  katika Chuo hicho kwa kutumia mapato ya ndani ya VETA.

"Nimezindua Chuo hiki lakini sijaridhishwa na majengo, ni machache na hayana hadhi kwani Wizara imetoa hela kulingana na mahitaji  yenu, inakuwaje bado kuna changamoto za majengo? Natoa miezi sita mkamilishe kwa fedha zenu," alisisitiza Ndalichako.

Wakati huo huo Ndalichako amewashukuru Wananchi wa Ndolage na Mbunge wa Jimbo hilo  kwa  hatua ya kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha watoto na Vijana katika eneo hilo wanapata Elimu kwa kujitolea ardhi bure kwa ajili ya ujenzi huo na kuchangia fedha za vifaa.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, ameishukuru Wizara ya Elimu kwa ujenzi wa Chuo hicho na ameahidi kuhamasisha Wananchi kuandikisha Vijana wao kujiunga na Chuo hicho.

Akitoa salamu za VETA, Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Peter Maduki amesema Chuo hicho kitadahili wanafunzi 80 wa kozi za muda mrefu na wanafunzi 300 wa kozi fupifupi ambao wanatarajiwa kuanza mafunzo Januari mwaka 2020.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo hilo la Muleba kaskazini, Charles Mwijage ameishukuru Serikali kwa kujenga Chuo  hicho huku akiushauri uongozi wa VETA kuongeza mafunzo ya fani ya usindikaji mazao  kwani wananchi wa eneo hilo wamejikita katika kilimo.

Mafunzo mengine yatakayotolewa katika Chuo hicho ni ya fani za  Uashi, Ushonaji, Uhazili, Urembo na Uungaji wa Vyuma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni