Jumatano, 24 Mei 2017

Wasichana na Wanawake kuwezeshwa kupitia elimu


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji Dkt Leonard Akwilapo leo amefungua warsha ya kuanzishwa kwa mradi wa pamoja wa uwezeshaji wa wasichana na wanawake  kupitia elimu kwa lengo la kuwatafakarisha wilaya lengwa (Ngorongoro, Kasulu, Sengerema,micheweni na mkoani pemba) juu ya vikwazo vya elimu kwa wasichana katika maeneo yao na kubuni mikakati mbalimbali ya kukabiliana navyo ili wasichana wapate fursa ya kujiendeleza kielimu na kukuza fursa ya kuwa raia bora Zaidi.

Mradi huu wenye thamani ya dola za kimarekani milioni tano unafadhiliwa na shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea (KOICA) kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambapo unatarajiwa kuwanufaisha wasichana na wasichana 8,000 walioko shuleni na wasichana 600 walio nje ya shule, kwa kuwapatia fursa ya kuimarisha ujuzi wao wa msingi, ufundi na ujuzi wa kawaida ambao utawawezesha kuwa raia bora katika nchi yao na ulimwengu kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuchangia kikamilifu katiak maendeleo ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa ufunguzi Katibu Mkuu amesema Awamu ya kwanza ya mradi huu unalenga nchi tatu ambazo ni Tanzania, Mali na Nepal na utaratibiwa na Wizara ya elimu Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Wizara ya katiba na Sheria na kutekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni pamoja na UNFPA na UN Women.

Mradi huu ni sehemu ya mpango wa ulimwengu kupitia mashirika ya UNESCO, UNFPA na UN Women kwa ajili ya kuwawezesha wasichana kupitia elimu uliozinduliwa katika nchi sita duniani kote.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo akifungua warsha ya kuanzishwa kwa mradi wa pamoja wa uwezeshaji wa  Wanawake na Wasichana kupitia Elimu, mkutano ambao umefanyika jijini Dar es salaam hii leo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo akifuatilia Makala zilizoandaliwa kuonyesha namna Wasichana  na Wanawake wanavyofurahia kupata Elimu ya namna ya kujikinga na matatizo katika jamii yanayoambatana na mila potofu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni. (UNESCO.)

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha mara baada ya ufunguzi wa warsha ya kuanzishwa kwa mradi wa pamoja wa uwezeshaji wa wasichana na Wanawake kupitia Elimu.



Jumanne, 23 Mei 2017

Ushiriki wa Waziri wa Elimu Sayansi, na Teknolojia katika Mkutano Mkuu wa 18 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakati wa Mkutano Mkuu wa 18 wa Wakuu wa Nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliifanyika hivi karibuni Ikulu jijini Dar Es Salam, Tanzania.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakibadilishana uzoefu na baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 18 wa Kawaida  wa Wakuu wa Nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika mwishoni mwa wiki Ikulu, jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.



 Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki likiwa katika picha ya pamoja na viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa Mkutano Mkuu wa Kawaida wa 18 uliofanyika hivi karibuni Ikulu jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa na baadhi ya Mawaziri wa Tanzania wanaounda Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia Mkutano Mkuu wa 18 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo uliofanyika hivi karibuni, Ikulu jijini Dar es Salaam, Tanzania

Ijumaa, 12 Mei 2017

MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA WIZARA YA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA-MOROGORO


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Saimon Msanjila amezindua mkutano wa 24 wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ulioanza leo katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine mjini Morogoro ambapo amewaasa watumishi kufanya kazi kwa weledi na maarifa zaidi ili kuleta ufanisi utakaokuwa na tija.

 Profesa Msanjila amesema ili kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu ni lazima watumishi kubadilika na kufanya kazi kwa kujituma na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.

Profesa Msanjila  amesisitiza kuwa wizara ina wajibu wa kuhakikisha nchi inakuwa na elimu bora ili kupata wahitimu na wataalam watakaowezesha nchi kufikia lengo la kuwa na  uchumi wa viwanja.

Aidha, amewataka wajumbe wa mkutano kujielekeza zaidi katika mbinu na mikakati ya utekelezaji kwa kushirikiana na uongozi wa Wizara ili kukamilisha malengo ya mwaka 2016/17 na malengo mapya ya mwaka 2017/18.