Jumanne, 31 Oktoba 2017

Naibu Waziri Ole Nasha atoa maagizo kwa Bodi ya Mikopo na Tume ya Vyuo Vikuu


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amezitaka Tume ya Vyuo Vikuu na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kuhakikisha wanakamilisha taratibu za udahili na utoaji mikopo kwa wakati ili wanafunzi wanaojiunga na masomo ya elimu ya juu waanze mara moja bila kuchelewa.

Naibu waziri Ole Nasha ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika Taasisi hizo ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kuteuliwa ili kujionea utendaji kazi wa taasisi hizo.

Naibu Waziri amesema serikali imeidhinisha takribani shilingi bilioni 427 kwa ajili ya wanafunzi 122,000 wanaoanza na kuendelea na masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2017/18.
“lengo la Serikali ni kuona wanafunzi wote wanaanza masomo bila kuchelewa na katika kutekeleza hilo tayari serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 147 kwa Bodi ya Mikopo kwa ajili ya robo ya kwanza ya kuwawezesha wanafunzi wenye sifa na vigezo wanaoanza na wale wanaoendelea masomo yao hivyo hatutegemei kusikia malalamiko yoyote kutoka kwa wanafunzi wanaostahili mikopo hiyo” alisisitiza Ole nasha

Pia ameitaka Bodi kutoa taarifa kwa umma majina yote ya wadaiwa sugu wa mikopo ambao mpaka sasa hawajaonyesha utayari wa kurejesha mikopo hiyo kwani lengo la serikali ni kuona bodi ya mikopo inaanza kujiendesha yenyewe badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.
Katika hatua nyingine Mhe. Ole Nasha ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu nchini kuhakikisha mfumo unaotumika kudahili wanafunzi  kutochelewesha wanafunzi kupata mikopo kwa wakati ili kuwawezesha kujiunga  na vyuo mapema.

Ole Nasha ameitaka Taasisi hiyo kushirikiana na wanafunzi kwa karibu katika kipindi hiki cha udahili ili kufikia Novemba 2 mwaka huu zoezi hili la udahili liwe limekamilika.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni