Jumanne, 31 Oktoba 2017

TEWW yatakiwa kutekeleza  majukumu yake

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Ole Nasha ameitaka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kimuundo badala ya kufikiria kufanya miradi ambayo imekuwa ikiwaondoa kwenye mwelekeo wa malengo ya uanzishwaji wa Taasisi hiyo.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam alipotembelea Taasisi hiyo  ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kuzitambua taasisi zilizo chini ya wizara pamoja na utendaji wa majukumu yake.
Akiwa katika Taasisi hiyo amesema nchi bado inaihitaji Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima pamoja na aina ya elimu ambayo inatolewa na taasisi hiyo, hivyo ameitaka taasisi hiyo  kutekeleza majukumu yake iendane na hali halisi ya mazingira ya elimu.
Ole Nasha amesema ukiangalia utekelezaji wa miradi  hiyo inabaki kuitwa elimu ya watu wazima lakini namna inavyoendeshwa haziakisi uhalisia wake na badala yake zinabaki kuwa kama mifumo mingine ya utoaji wa elimu ya mfumo rasmi.

Naibu Waziri Ole Nasha akiwa katika taasisi hiyo amepata fursa ya kutembelea chumba cha Uchapaji vitabu  majarida, Karakana, Maktaba na idara ya Elimu ya masafa na Studio za kuandaa vipindi vya kuelimisha umma vya Elimu ya Watu Wazima.
Aidha, Naibu Waziri ametembelea Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Elimu, Habari, utamaduni  ya UNESCO na kuwataka kuitisha kikao cha wadau wanaohusika na Tume hiyo ili kuzungumzia changamoto za kimfumo na muundo zinazoikabili taasisi hiyo.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni