Alhamisi, 5 Oktoba 2017

Waziri Ndalichako azindua Bodi ya Wakurugenzi HESLB na Baraza la TET

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknnolojia Prof. Joyce Ndalichako amelitaka  Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania na Bodi ya wakurugenzi ya Bodi ya mikopo ya Wanafunzi  wa elimu ya juu kufanya kazi kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu za kazi.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa bodi hizo ambapo amezitaka pia kuhakiksha zinarudisha hadhi ya Taasisi  za serikali wanazozisimamia katika kutoa huduma kwa wananchi kwa kuweka miongozo ya utendaji kazi na kuhakikisha wanaisimamia miongozo hiyo ili kuleta ufanisi katika kazi.

Ndalichako amezitaka bodi hizo kuhakikisha zinatembea katika ahadi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli za kuhakikisha zinawasaidia wanyonge kupata Elimu bora.

Waziri Ndalichacho amelitaka Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania kuhakikisha vitabu vyote vyenye makosa vinarekebishwa na kwamba bodi ijiridhishe na mfumo na utaratibu utakaotumika katika kuvirekebisha vitabu hivyo.

Baraza hili ambalo litahudumu kwa miaka mine (4) kuanzaia septemba 2017 hadi septemba 2021 limetakiwa pia kusimamia Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma vizuri kwa sababu kumekuwa na upotoshaji kuhusiana na Taasisi lakini pia amewataka kuhakikisha kunakuwa na vipindi vya kuelimisha namna Taasisi inavyotekeleza majukumu yake. 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania Profesa Bernadetta Kilian amesema atahakikisha Taasisi inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kwamba maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi ili kukidhi matarajio ya watanzania. 
Hakuna maoni:

Chapisha Maoni