Jumamosi, 6 Januari 2018

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
 


Anwani ya Simu: “ELIMU”
DAR ES SALAAM
Simu: 0262963533,
Tovuti:www.moe.go.tz


 
Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma
S. L. P.  10
40479 DODOMA






TAARIFA KWA UMMA

Ndugu Wanahabari,
Kama ambavyo wengi wenu wanafahamu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea na programu yake ya ukarabati mkubwa wa shule kongwe za Sekondari nchini. Programu ambayo itahusisha jumla ya shule kongwe 89. Katika awamu hii ya kwanza ambayo imetekelezwa kwa miaka miwili sasa, yaani mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18, jumla ya shule 46 kati ya 89 zipo kwenye mpango wa ukarabati huu. Taarifa ya programu hii ya ukarabati ni kama ifuatavyo:

  • Shule 10 za sekondari ambazo ni Mpwapwa, Musoma Ufundi, Mtwara Ufundi, Ifakara, Kantalamba, Tanga Ufundi, Ifunda Ufundi, Moshi Ufundi, Bwiru Wavulana na Kibiti zinaendelea kukarabatiwa kwa usimamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST). MUST ni taasisi ya kielimu, kwa hiyo wamekuwa makini sana na ratiba za shule. Shule zote hizi ziko katika hatua za mwisho za ukarabati na wanafunzi wanaendelea na masomo kama kawaida;
  • Shule za Sekondari za Iyunga, Chidya, Tambaza, Zanaki na Kisutu zinakarabatiwa chini ya Uongozi wa Shule na Bodi za Shule kwa usimamizi wa Halmashauri za Wilaya zao. Nazo pia ukarabati unaendelea vizuri sana. 
  • Shule ya sekondari ya Ndwika ambayo iko Wilaya ya Masasi, inajengwa upya chini ya Halmashauri baada ya taarifa ya wahandisi kubaini kuwa majengo yake hayawezi kufanyiwa ukarabati. 
  • Shule za Sekondari za Nyakato na Ihungo nazo pia zinajengwa upya kufuatia kuharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi lililotokea katika Mkoa wa Kagera mwezi Septemba, 2016. Na kwa upande wa Shule ya Sekondari ya Rugambwa, hii inajengewa nyumba 8 za walimu ambazo zilibomoka kutokana na tetemeko hilo;
  •  Vilevile Wizara kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania inakarabati Shule za Sekondari 17 ambazo ni : Ilboru, Same, Pugu, Mwenge, Nganza, Mzumbe, Kilakala, Tabora Wavulana, Tabora Wasichana, Msalato, Dodoma, Ruvu, Korogwe, Bwiru Wasichana, Sengerema, Bihawana na Kondoa Wasichana. Katika ya hizi mpaka sasa shule 10 zimeshakamilika na saba zitaanza kukarabatiwa hivi karibuni bila kuathiri masomo.
  •  Shule za Sekondari 9 ambazo ni Jangwani, Azania, Kibaha, Kigoma, Tosamaganga, Malangali, Milambo, Minaki na Nangwa zinaendelea kukarabatiwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Majengo Tanzania – TBA ambazo zipo kwenye hatua mbalimbali za ukarabati, ambapo shule ya Songea Wasichana bado haijaanza kukarabatiwa.
  •  Ndugu Wanahabari kama mnavyotambua shule zetu zinafunguliwa kesho kutwa tarehe 8 Januari.
  • Wizara baada ya kufanya tathmini ya kina imegundua kuwa kwenye shule zinazokarabatiwa na TBA kumekuwa na tatizo la ukamilishwaji wa miradi katika muda uliopangwa. Miradi yote iko nyuma ya ratiba. Na mbaya zaidi ni kwamba baadhi ya shule haziko tayari kabisa kupokea wanafunzi na wakaendelea na masomo yao kwa ukamilifu. Yaani mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji hayajakamilika.
  • Hivyo basi baada ya mashauriano na wenzetu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI tumekubaliana kuhairisha kuanza kwa muhula wa kwanza kwa shule za Milambo, Jangwani na Azania.
  • Kwa shule hizi muhula wa kwanza utaanza tarehe 22 Januari 2018.
  • Ratiba za masomo katika shule hizi itarekebishwa ili wiki hizi mbili ziweze kufidiwa. Utaratibu wa kawaida ni kufidia muda huu wakati wa likizo fupi na likizo ndefu ya mwezi ya mwezi Julai.


Wizara kwa kushirikiana na Serikali za Mikoa na Halmashauri husika itafanya usimamizi wa karibu kuhakikisha kuwa shule hizi zinakamilika katika kipindi hiki cha wiki mbili.

Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza kwa wazazi/walezi na wanafunzi wanaosoma na waliochaguliwa kujiunga katika kidato cha kwanza katika shule hizi. Natumaini mnatambua nia njema ya Serikali ya kutaka kuimarisha mazingira ya shule hizi ambazo zilikuwa zimechakaa sana.

Nachukua fursa hii pia kuwaagiza Wakala wa Majengo, TBA, kutekeleza majukumu yao kulingana Mikataba tuliyoingia nao. Pamoja na shule hizi Kongwe pia tumewapa kazi za ujenzi wa Kampasi ya MUHAS-Mloganzila. Matarajio yetu ni kwamba Kampasi hii itachukua wanafunzi wa kwanza mwaka huu. Nawaagiza TBA kuongeza juhudi pale Mloganzila ili lengo hili likamilike.

Maelekezo ya Waziri wangu Mhe. Prof. Ndalichako ni kuhakikisha kuwa tunafanya usimamizi wa karibu ili miradi yote ya TBA ianze kwenda kulingana na Mikataba. Tutafanya hivyo wakati pia tunaangalia taratibu za kisheria ili kama kuna hatua zozote muafaka ziweze kuchukuliwa ili malengo yakamilike kulingana na matarajio.

Ninawashukuru sana.

Dkt. Leonard D. Akwilapo
KATIBU MKUU
06 Januari 2018

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.