Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichoko ameishukuru Serikali ya Watu wa China
kwa kukubali ombi lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dk John Magufuli la kufadhili wataalam wa sekta ya Afya.
Waziri Ndalichako ametoa kauli
hiyo hii leo alipotembelewa na Balozi wa China nchini Tanzania Wang Ke
aliyefika katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kufanya mazungumzo kuhusu utaratibu wa kupata wanafunzi watakaofaidika na
ufadhili huo.
Balozi Wang Ke amesema
baada ya Rais wa China kupata maombi hayo ametoa ufadhili wa Serikali yake kwa
wanafunzi 20 wa Kitanzania watakaopata ufadhili wa masomo katika Sekta ya Afya
kutoka Serikali ya China kwa mwaka wa masomo wa 2018/2019 katika ngazi za
Uzamili na Uzamivu.
Aidha, Balozi Wang Ke
amesema mbali na ufadhili huo pia Serikali ya China itaendesha Mpango wa
Mafunzo kwa wataalamu wengine 20 mpaka 30 wa Sekta ya Afya kwa muda wa mwezi
mmoja nchini China, hivyo amemuomba Waziri wa Elimu kusaidia katika
kuratibu upatikanaji wa Wanafunzi na aina ya mafunzo ambayo yatasaidia katika
kutatua changamoto katika Sekta ya Afya.
Katika hatua nyingine
Waziri Ndalichako amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya
Korea Song Geum – Young kwa lengo la kujadili ujio wa wabunge kutoka
Bunge la Korea kwa ajili ya kutoa msaada katika Hospitali ya Tiba na Taaluma ya
Mlongazila.
Waziri Ndalichako
amemwambia balozi huyo kuwa Serikali bado inaendelea kutafuta fedha kwa ajili
ya kujenga mbiundombinu ya kuwezesha wanafunzi na wauguzi kuishi karibu na
hospitali ya Taalum na Tiba ya Mlongazila.
Waziri amesema kwa sasa
serikali ipo katika ujenzi wa awamu ya kwanza ya Miundombinu itakayowezesha
wanafunzi wapatao 1500 kuishi karibu na hospitali hiyo.
Waziri Ndalichako amesema
Hospitali hiyo imejengwa kwa lengo la kuongeza udahili wa wanafunzi mpaka
kufikia wanafunzi zaidi ya 10,000 hivyo bado Miundombinu itakayowezesha
kuchukua idadi hiyo ya wanafunzi pamoja na watumishi wa hospitali hiyo
inahitajika.
Naye Balozi wa Jamhuri ya
Korea amesema serikali yake bado itaendelea kusaidia katika uendeshaji wa
hospitali hiyo pamoja na miradi mingine katika Sekta ya Elimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya
Korea Song Geum – Young ofisini kwake ambapo kwa pamoja
walijadiliana namna bora ya kuisaidia uboreshaji wa Miundombinu ya Hospitali ya
Tiba na Taaluma ya Mloganzila.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.