Jumatatu, 12 Februari 2018

Katibu Mkuu Akwilapo asisitiza matumizi ya force akaunti kwa FDCs


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo leo amefungua mafunzo yanayoelekeza matumizi ya Force Akaunti kwa Wakuu wa Vyuo vya  Maendeleo ya Jamii- FDCs mkoani Morogoro na kusisitiza kuwa utaratibu huo umekuwa na thamani ya matumizi ya fedha, (value for money).
Akizungumza na Wakuu wa Vyuo, Wakufunzi, Maafisa Ugavi na Wahasibu kutoka Vyuo hivyo Katibu Mkuu Akwilapo amesema lengo ni kuwajengea uelewa wa namna ya kusimamia ukarabati ili kuhakikisha Vyuo na Wizara kwa pamoja vinapata thamani ya matumizi ya fedha.

Dk. Akwilapo ameeleza kuwa Force Akaunti  ni utaratibu wa manunuzi ya huduma unaotambulika Serikalini na umekuwa ukitumia sehemu kubwa ya bajeti yake katika ununuzi wa vifaa mbalimbali inayotumika katika ujenzi.

Dk. Akwilapo amesema  lengo la kutumia utaratibu huo ni kupunguza gharama za ujenzi na ukarabati pamoja na kufanya utekelezaji wa mradi kukamilika kwa wakati, kukabiliana na  dharura zinazohitaji kuchukuliwa hatua za haraka pamoja na kuiwezesha taasisi husika kufanya kazi ya ujenzi na ukarabati kwenye taasisi yake pale ambapo ujenzi ni shughuli za kila siku katika Taasisi hiyo.

Ameongeza kuwa Wizara ilitumia wataalam wake katika ujenzi na ukarabati ambapo fedha iliyotumika kwa ajili ya kazi zilionekana kuwa kidogo.

 "Kwa majaribio force Akaunti ilitumika katika halmashauri 129 kujenga madarasa, mabweni, mabwalo, maabaara, Ofisi za walimu, nyumba za walimu  na umeonesha mafanikio makubwa  mahali ambapo kwa kutumia mkandarasi wastani wa shilingi bilioni 2 hadi 3 zingetumika ila kwa utaratibu wa Force Account Wizara imeweza kutumia shilingi milioni 800 hadi bilioni 1 tu".alisema Dk.Akwilapo.

Kwa upande wake mratibu wa mradi wa ESPJ Dk. Jonathan Mbwambo amewataka Washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia mafunzo na pia kutumia fedha watakazopewa za ujenzi na ukarabati kama zilivyokusudiwa.

Kati ya vyuo 55 vya FDCs vyuo 20 vitakarabatiwa na kujengwa katika awamu hii ya kwanza ambapo upembuzi yakinifu unatarajiwa kuanza mapema wiki ijayo.
Mafunzo hayo yameratibiwa na mradi wa kukuza stadi za kazi na ajira, ESPJ.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.