Ijumaa, 2 Machi 2018

Wakufunzi watakiwa kuzingatia uadilifu na kuweka mbele maslahi ya Taifa.


Naibu Katibu Mkuu Dk.Ave Maria Semakafu amewataka Wakufunzi nchini kuwa waadilifu na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele siku zote wanapotekeleza majukumu yao ya kazi.

Dk.Semakafu ametoa rai hiyo mkoani Mwanza wakati akifungua mafunzo ya TEHAMA kwa wakufunzi wa Vyuo vya Ualimu yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu Butimba mkoani humo.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema lengo la mafunzo ni kuwa na maudhui yenye viwango vya ubora unaotakiwa ili kuleta ufanisi katika kujifunza na kufundisha hususan katika  kuandaa Walimu. 

Dk. Semakafu amesisitiza kuwa  mafunzo hayo yatawajengea umahiri na hatimaye kuwa na rasilimali watu yenye maarifa na umahiri kwa ajili ya uzalishaji na hatimaye kukuza uchumi na kufikia malengo ya nchi kwa kuwa na uchumi wa kati na Uchumi wa Viwanda ifikapo 2025. 

" Zipo  changamoto katika Sekta  ya Elimu, sasa lazima tuzitafutie ufumbuzi wa  namna ya kuzikabili kwa kutumia mfumo wa kidigitali ili kuboresha ufundishaji na pia kubadilishana taarifa na maarifa," amesema Dk. Semakafu.

Kwa upande wake mratibu wa Mradi huo  Ignas Chonya amesema Mradi wa Teacher Education Support Project (TESP) utawezesha kufanikisha  umahiri wa mwalimu kupitia mafunzo kazini ya wakufunzi katika maeneo mbali mbali ikiwemo mafunzo ya TEHAMA, mafunzo endelevu katika masomo wanayofundisha, mafunzo ya Uongozi wa Elimu,  ambayo ndiyo nguzo muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa Elimu bora hapa nchini.

Wakufunzi walioshiriki Mafunzo hayo ya Siku Tisa ni kutoka katika Chuo cha Ualimu Butimba,Tabora, Shinyanga, Ndala,Murutunguru, Bunda, Katoke, Tarime,Kasulu na Kabanga.

Mradi wa TESP unatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Canada kupitia Idara yake DFATD kwa ajili ya kugharamia mradi huo kwa kuweka kipaumbele cha kuleta mabadiliko chanya katika Elimu ya Ualimu.
 Naibu Katibu Mkuu Dk. Avemaria Semakafu akisalimiana na viongozi mbalimbali baada ya kuwasili katika Chuo cha Ualimu Butimba kilichopo mkoani Mwanza.

 Baadhi ya Wakufunzi kutoka Vyuo 10 vya Ualimu hapa nchini wakishiriki mafunzo ya TEHAMA, yanayoendeshwa na  TESP.

Naibu Katibu Mkuu Dk. Avemaria Semakafu akionyesha rasimu ya kitabu ambacho ndiyo mwongozo katika kujifunzia TEHAMA kwa Wakufunzi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni