Alhamisi, 30 Agosti 2018

DK. SEMAKAFU: WATHIBITI UBORA WA SHULE HAKIKISHENI ELIMU INAYOTOLEWA NCHINI INAKIDHI VIGEZO.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. AveMaria Semakafu amewataka Wathibiti Ubora wa Shule nchini kutumia taaluma zao kuhakikisha kwamba Elimu inayotolewa nchini ni ile inayozingatia vigezo, kanuni na taratibu za nchini na si vinginevyo.

Dk Semakafu ameyasema hayo Mkoani Morogoro wakati wa kufungua mafunzo ya Muongozo wa Huduma ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira Shuleni (SWASH) kwa wathibiti ubora wa Shule wa Wilaya ambapo amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kujua changamoto zinazokwamisha upatikanaji wa Elimu bora katika maeneo yao.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu akizungumza na Wathibiti Ubora wa Shule wa Wilaya (hawapo pichani) wanaoshiriki mafunzo ya Muongozo wa Huduma ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira Shuleni (SWASH) yanayofanyika katika Chuo Cha Ualimu Morogoro mkoani Morogoro kuanzia Agosti 27 hadi 31, 2018

Dk. Semakafu pia amewataka Wathibiti ubora kufanya utafiti, kuainisha changamoto zilizopo katika maeneo mbalimbali ya shule pamoja na kuandaa ripoti na mapendekezo ambayo wanadhani Programu ya SWASH itaweza kusaidia kutatua.

“Mafunzo haya mliyoyapata yaende kuwasaidia katika kufanya tafiti, kuanisha changamoto zilizopo katika maeneo mbalimbali ya shule pamoja na kuandaa ripoti na kutoa mapendekezo, ambayo yatasaidia kuimarisha utendaji na kuwashirikisha wale ambao hawajapata mafunzo hayo kwa kuwa sasa mmekuwa na uelewa mpana kuhusiana na masuala ya huduma ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira Shuleni,” amesema Semakafu


Baadhi ya Wathibiti Ubora wa Shule wa Wilaya wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu wakati akifungua mafunzo ya Muongozo wa Huduma ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira Shuleni (SWASH), mafunzo ambayo yanafanyika  mkoani Morogoro kuanzia Agosti 27 hadi 31, 2018.

Amewataka pia kuhamasisha upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo wanayofanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Elimu ya afya na mazingira safi yanapatikana Shuleni ili watoto waweze kupata Eimu bila changamoto yoyote.

Mafunzo ya Muongozo wa Huduma ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira Shuleni   yameshirikisha Wathibiti Ubora wa Wilaya 48 kutoka Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Iringa, Singida na Manyara.
Wathibiti Ubora wa Shule wa Wilaya wanaoshiriki mafunzo ya Muongozo wa Huduma ya Maji, Afya na Usafi wa Mazingira Shuleni (SWASH) wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu mkoani Morogoro

Maoni 1 :

  1. Hongera GCU,Asante Dr.Semakafu kwa ujumbe na maagizo mzuri.

    JibuFuta

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.