Jumatano, 29 Agosti 2018

SERIKALI HAITAMVUMILIA ATAKAYEFANYA SHULE KUTOKUWA SEHEMU SALAMA KWA WANAFUNZI


Serikali imesema haitavumilia mtu yeyote ambaye atafanya matendo yatakayoashiria kwamba shule si mahala salama kwa mwanafunzi, pamoja na kuwatia hofu wazazi waogope kuwaruhusu watoto kwenda kupata Elimu.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Profesa Joyce Ndalichako siku moja baada ya kuwepo kwa taarifa juu   mwalimu Respicius Patrick wa Shule ya Msingi Kibeta iliyopo mkoani Kagera kumpiga hadi kumsababishia kifo mwanafunzi Sperius Eradious mwenye umri wa miaka 13 wa darasa la tano.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwakabidhi sheria na kanuni Wajumbe wa Bodi mpya ya Baraza la Mitihani Tanzania katika uzinduzi wa Bodi hiyo uliyofanyika jijini Dar es Salaam

Waziri Ndalichako amesema Shule ni mahala salama kwa wanafunzi kujifunza, kitendo hicho kilichofanywa na mwalimu huyo ni kinyume na malengo ya serikali  ambayo imekuwa ikiboresha Elimu na kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha watoto wanapata Elimu bora na tena kwenye mazingira mazuri.

“ Suala ambalo limefanywa na huyu Mwalimu ni kinyume kabisa na maadili ambayo Mwalimu anatakiwa kuwa nayo, kwa umri ambao mwanafunzi alikuwa nao Mwalimu ndiyo alitakiwa awe msaada mkubwa wa kumuelimisha na kumfundisha mwanafunzi,niendelee kuwaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu, wakati vyombo vya Sheria vinaendelea kufanya kazi yake,” alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wataalamu wa waandaaji wa walimu wa somo la hesabu (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam, ambapo amewataka walimu kuangalia namna nzuri ya kumuandaa mwanafunzi kupenda somo la hesabu.

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amewataka wataalamu wa somo la hesabu kuangalia namna bora ya kuimarisha ufundishaji wa somo la hilo ili kuwezesha walimu  kufundisha na kuhamasisha wanafunzi kupenda somo hilo.

Waziri Ndalichako amesisitiza hilo katika kongamano la tano la wataalumu wanaoandaa walimu wa somo la hesabu Barani Afrika kuwa ni muhimu kuangalia mbinu wanazopewa walimu wanaofundisha somo hilo kama zinawasaidia kufundisha kwa kutumia njia shirikishi.
Kongamano linalowakutanisha wataalamu wa hesabu linafanyika jijini Dar es Salaam kwa kwa lengo la kuimarisha ufundishaji wa somo la hesabu ambapo mgeni rasmi katika kongiomano hilo ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.  

Kupitia kongamano hilo amewataka kuangalia pia namna nzuri ya kuwezesha walimu wa hesabu kuondoa dhana potofu kwa wanafunzi kuwa somo hilo ni gumu, na kusisistiza kuwa mwanafunzi akielewa hesabu inamuwezesha kumudu masomo mengine vizuri kutokanana kutumia zaidi mantiki katika kutatua hesabu.

Akiwa jijini Dar es salam Waziri Ndalichako pia amezindua bodi ya Baraza la Mitihani la Tanzania ambapo amewataka wajumbe wa Baraza hilo kuhakikisha mitihani inaandaliwa katika ubora unaotakiwa na wahakikishe wanakuwa  na umakini katika uendeshaji wa Kazi zote zinazohusiana na mitihani.

Maoni 1 :

  1. Hongera sana GCU & IT kwa kutuhabarisha.
    Asante kwa Mhe.Waziri kwa kumweka vizuri suala la salama wa mtoto.
    Wito kwa wakuu wa shule sote, waimarishe huduma ya malezi shulen

    JibuFuta