Serikali imelitaka Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha Vyuo inavyovisimamia vinahuisha
mitaala yake kila baada ya miaka mitatu kwa mujibu wa sheria ili kile
kinachofundishwa kiweze kuendana na mahitaji halisi ya soko kwa sasa ikiwa ni
pamoja na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia.
Kauli hiyo ya Serikali
imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha jijini Dar Es Salaam alipofanya ziara
katika Taasisi hiyo ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kutembelea Taasisi zilizo
chini ya Wizara na kuona namna wanavyotekeleza majukumu yao.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na
watumishi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi NACTE (hawapo pichani)
alipofanya ziara katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam kuona namna
wanavyotekeleza majukumu yao.
Ole Nasha alisema ufundi ni
taaluma ambayo inabadilika kila siku hivyo ni vyema mitaala ikahuishwa ili kozi
zinazotolewa ziendana na ushindani wa soko la ajira.
Pia Naibu Waziri Ole Nasha amelitaka Baraza hilo
kuendelea kufanya ukaguzi wa vyuo vyake na kuvifutia usajili vyuo vyote ambavyo
havifuati sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kuvichukulia hatua
vinavyoendelea kufanya makosa kwa mujibu wa sheria.
“Baraza la Taifa la Elimu ya
Ufundi (NACTE) tangu mwaka 2016 imefungia vyuo 74 ambavyo havifuati taratibu wakati
mwaka huu vyuo 3 vimefungiwa huku vingine 21 vikizuiliwa kutoa baadhi ya kozi
hii ni kutokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyo nayo ya
kuhakikisha Elimu itolewayo ni bora na sio bora Elimu” aliongeza Naibu Waziri
Ole Nasha.
Watumishi
wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha alipofanya ziara katika Taasisi
hiyo iliyopo jijini Dar es salaam
Katika hatua nyingine
ameipongeza NACTE kwa kusimamia vizuri udahili wa wanafunzi kwa mwaka huu ikiwa
ni pamoja na kutengeneza mifumo 14 ya TEHAMA ambayo imesaidia zoezi la udahili
kufanyika kwa ufanisi hatua iliyopelekea kuongeza idadi ya wanafunzi elfu kumi
zaidi kutoka ile ya mwaka jana ambayo walidahili wanafunzi 110,000.
Amesema Serikali ya Awamu ya
Tano ni Serikali ambayo imejipambanua katika kufikia uchumi wa kati na wa
Viwanda ambao ili uweze kufanikiwa uanahitaji mafundi waliosoma vizuri, hivyo
elimu ya ufundi ni moja ya vipaumbele vya Serikali na kuzitaka Mamlaka hizo kusimamia elimu itolewayo ili tolewe kama inavyostahili.
Naibu Waziri amehitimisha
ziara yake ya siku moja jijini Dar es Salaam kwa kutembelea Mamlaka ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi stadi VETA ambapo amewataka kuandaa vijana ambao ni mahiri na
wabobezi katika fani mbalimbali watakaofanya kazi katika viwanda ili kujenga
uchumi wa viwanda.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa katika picha ya
pamoja na viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Stadi VETA Makao makuu jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.