Serikali imeahidi kutoa kiasi cha
Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya kujenga na kukarabati Miundombinu mbalimbali
katika shule ya msingi Mwisenge aliyosoma Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K.
Nyerere iliyopo manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako mara baada ya kutii
maelekezo yaliyotolewa na Rais John Magufuli ya kuitembelea shule hiyo na kufanya
tathmini kwa lengo la kuikarabati ili iendane na hadhi ya Baba
wa Taifa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako
akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima wakiwa wamekaa kwenye dawati
alilokuwa anatumia Baba wa Taifa Mwalimu Jullius Nyerere wakati akisoma katika shule
ya Msingi Mwisenge iliyopo manispaa ya Musoma, Mkoani Mara.
Waziri Ndalichako amesema,
kipaumbele cha Serikali ya awamu ya Tano ni Elimu, hivyo amemwelekeza Mkuu wa
mkoa huo Adam Malima kuhakikisha kuwa fedha ambazo zitaelekezwa katika shule
hiyo basi zisimamiwe ili zifanye kazi iliyokusiduwa na si kutumika vinginevyo.
“Rais John Magufuli akiwa katika
ziara zake alifika na kuona kuwa shule hii inahitaji kuboreshwa hivyo
alinielekeza nifike na kufanya tathmini kwa lengo la kuboresha Miundombinu ya
Shule hii, sasa Mkuu wa mkoa mimi na wewe tuhakikishe uboreshaji unafanyika
tena kwa kiwango kitakachoendana na hadhi ya Baba wa Taifa letu,” alisisitiza
Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu na Mkuu wa mkoa wa Mara
wakiwa nje ya bweni alilokuwa analala Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere
katika shule ya msingi aliyokuwa anasoma ya Mwisenge iliyopo manispaa ya Musoma.
Waziri Ndalichako amesema fedha
hizo zitatumika kujenga mabweni mawili mapya, vyumba vitano vya madarasa,
kukarabati Nyumba za walimu na kuboresha Miundombinu ya maji.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa huo
Adam Malima ameahidi kusimamia fedha zitakazotolewa kwa ajili ya kuboresha
Miundombinu katika shule hiyo na kuwa shule hiyo itakuwa mfano na pia
kumbukumbu nzuri kwa Taifa.
Waziri Ndalichako pamoja na
viongozi mbalimbali wa mkoa huo pia wametembelea Shule ya sekondari ya Ufundi
Musoma, Shule ya sekondari Mara na Chuo Kikuu Cha kilimo na Teknolojia cha
Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani Butiama kwa lengo la kukagua hali ya
Miundombinu katika Taasisi hizo.
Darasa ambalo Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K.
Nyerere alilitumia kwa ajili ya kusoma kuanzia mwaka 1934 - 1936, shule hiyo
ipo kwenye manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.