Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote
nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 2 ya bajeti zao kwa ajili ya
kuhudumia watu wenye ulemavu na kuwa suala hilo lipo kisheria.
Waziri
Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe
duniani ambayo Kitaifa hapa nchini yamefanyikia Mkoani Mwanza.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na
Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya Elimu
Maalumu wa Wizara hiyo Adamson Shimbatano aliyeshika Fimbo Nyeupe wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe duniani ambayo kitaifa yamefanyikia mkoani
Mwanza.
Ndalichako
amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Magufuli
imeendelea kuboresha mazingira ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na
kutoa ajira na kuwa katika ajira za mwaka jana walimu 70 wasioona
waliajiriwa.
“Niwahakikishie
Watanzania kuwa Rais John Magufuli ni kiongozi anaejali sana watu wenye ulemavu
ndiyo maana wapo viongozi wenye ulemavu aliowateua kushika nafasi mbalimbali za
uongozi katika Serikali yake wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Mabalozi,
na wengine ili wamsaidie katika kutekeleza majukumu ya kuliletea Taifa
Maendeleo,” alisema Ndalichako.
Waziri
Ndalichako pia amewataka Wazazi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wasioona na
badala yake wahakikishe watoto wote waliofika umri wa kwenda Shule
wanaandikishwa kwa kuwa hivi sasa Elimu msingi inatolewa bila malipo na kuwa
ulemavu siyo kikwazo cha Maendeleo.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea msaada wa Fimbo
Nyeupe kutoka kwa mmoja Wafanyabiashara mkoani Mwanza, ili fimbo hizo zigaiwe
kwa watu wasioona walioshiriki maadhimisho hayo mkoani Mwanza.
Akizungumza
katika Maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu nchini
Tanzania Benedict Louis amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa
uongozi wake wa kutambua jitihada na uwezo wa watu wenye ulemavu na hivyo
kuwateua wenye ulemavu kushika nafasi mbalimbali.
Louis ameeleza kuwa Siku
ya Fimbo Nyeupe ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa kwa wasioona kutathmini
jitihada zinazofanywa na serikali katika kuleta ustawi kwa watu wenye ulemavu
na kuwa Fimbo hiyo ni nyenzo muhimu ambayo inamsaidia asiyeona
kutambua vikwazo vilivyo mbele yake.
Kauli mbiu
ya mwaka huu katika maadhimisho hayo ni “ Mafunzo ya TEHAMA kwa wasioona ni
nyenzo Shirikishi ya uchumi wa Viwanda.”
Watu
wasioona wakicheza mziki pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako wakati wa maadhimisho ya siku ya Fimbo Nyeupe ambayo kitaifa yamefanyikia
mkoani Mwanza na kauli mbiu katika maadhimisho hayo ni mafunzo ya TEHAMA kwa
wasioona ni nyenzo shirikishi ya uchumi wa Viwanda.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.