Serikali imewataka walimu wote nchini kuacha
kufanya vitendo vya udanganyifu wakati wa mitihani huku ikiwataka wanafunzi
kuhakikisha wanatoa taarifa kuhusu vitendo vya udanganyifu vinapokuwa
vinatokea.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa sherehe za kuadhimisha
miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule ya sekondari Don Bosco Didia iliyopo mkoani
Shinyanga.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako akiangalia maonesho ya picha na maandishi mbalimbali
kuhusu mwanzilishi wa Shule ya Sekondari ya Don Bosco ambayo ilianzishwa mwaka
1993-2018 na kuwa sasa imetimiza miaka 25.
Waziri Ndalichako amesema Serikali
inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Mashirika ya kidini katika
kuwaandaa vijana kitaaluma na kinidhamu na ndiyo maana hakuna vitendo vya
udanganyifu katika mitihani kwenye shule hizo kwa kuwa wanafunzi wanaandaliwa
vya kutosha pia wana maadili.
“Nichukue fursa hii kuwasihi sana
walimu nchini kote kuacha kufanya vitendo vya udanyifu wakati wa mitihani kwa
sababu tunawaharibu watoto na
tunatengeneza vijana ambao hawana uwezo kitaaluma, kama tunawafanyia mitihani
wakija kupata kazi pia tutawafanyia kazi?
“Nimependa Moto wa shule hii ya
Don Bosco Didia kuwa ni kulea, kuwafunza nidhamu watoto kwa lengo la kutimiza
ndoto zao naunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi wa shule hii sasa pia ni
vyema na shule nyingine zikaiga,” alisisitiza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako akipokea picha ya mfano wake ambayo imechorwa na mwanafunzi wa
shule ya Sekondari ya Don Bosco mkoani Shinyanga wakati wa kuadhimisha miaka 25
tangu shule hiyo ianzishwe.
Waziri Ndalichako ameihakikishia
Shule ya Sekondari ya Don Bosco kuwa Serikali iko pamoja kushirikiana na
shule hiyo kwa kuwa mambo wanayoyafanya wanaunga mkono juhudi za Serikali ya
awamu ya Tano.
Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab
Telack ameisifu shule hiyo ya Don Bosco kwa kuendelea kufanya vizuri katika
mitihani ya kidato cha nne na kuwa mkoa unajivunia sana kuwepo kwa shule hiyo
ambapo amewasisitiza wanafunzi kuhakikisha wanaendelea kushirikiana ikiwa ni
pamoja na kusoma kwa makundi pamoja na kuwasaidia wale ambao uwezo wao ni
mdogo.
Waziri Ndalichako
akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa
shule ya sekondari Don Bosco Didia iliyopo mkoani shinyanga.
Katika kuadhimisha miaka 25 tangu
kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 1993 Baba Vicent alisimikwa rasmi
kuwa Baba wa kiroho kwa ajili ya shule hiyo ya Sekondari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.