Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha amewataka viongozi kuanzia
ngazi ya mkoa hadi vijiji nchini kote kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza darasa
la saba hawaondoki katika maeneo yao
kwenda kufanya kazi za ndani wakati wakisubiri matokeo ya kuhitimu
darasa la saba, kwani kufanya hivyo kunawaondolea fursa ya kuendelea na masomo pindi wanapofaulu.
Ole Nasha ametoa agizo hilo
mkoani Manyara wakati akizungumza na viongozi hao kuhusu hali ya Elimu mkoani
humo ambapo amewataka kusimamia kwa ukaribu suala hilo ili kutokatisha ndoto za
watoto hao na kwamba wale wanaofanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa
dhidi yao.
"Hakikisheni watoto
wanaposubiri matokeo hawasafirishwi kwenda kwenye maeneo mengine kwa ajili ya
kufanya kazi za ndani, kumekuwa na tabia za kuwarubuni watoto hata wanapofaulu
na kutakiwa kurejea kwa ajili ya masomo hawarejei, Katika hili pia wazazi msiwe
sehemu ya kuchangia watoto wenu kwenda mjini kwa kuwa tu wanawatumia fedha kwa
ajili ya matumizi bali hakikisheni mnawasimamia vyema na kuwapeleka shule pindi
matokeo yanapotoka na kuonekana wamefaulu," alisisitiza Naibu waziri Ole
Nasha.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipokelewa na
Watendaji wa Mkoa wa Manyara wakati alipowasili mkoani hapo kwa ajili ya kupata
taarifa ya Elimu ya Mkoa huo. Naibu waziri huyo yuko Mkoani Manyara kwa ziara
ya siku tatu ikiwa ni muendelezo wa ziara zake ambazo amekuwa akizifanya
kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia pamoja na kuangalia hali ya Elimu katika mkoa husika.
Kiongozi huyo ameendelea
kuwasisitiza wazazi kuwa fursa za Elimu katika nchi yetu ni kubwa, ikizingatiwa
kuwa Elimu msingi ni bure hivyo hakuna kisingizio tena kuwa mtoto hawezi kusoma.
Amewataka viongozi hao
kutumia sheria kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule
wanaandikishwa ili kutokuwa na wimbi
kubwa la watoto wa mitaani wasiokwenda shule.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akitoa maelekezo kwa
Viongozi na watendaji wa VETA Manyara wakati wa kukagua karakana inayotumika na
wanafunzi wanaosoma kozi ya ufundi wa zana za kilimo (Agro Mechanics).
Awali Kaimu Katibu Tawala wa
Mkoa wa Manyara Arnold Msuya alimweleza Naibu waziri huyo kuwa mkoa kwa sasa
una mwamko mdogo wa Elimu hasa katika jamii ya wafugaji hali inayopelekea wazazi
kutowaandikisha shule watoto wenye umri wa kuanza shule.
Naibu waziri Ole Nasha pia ametembelea
Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi
stadi cha Mkoa Manyara na kuwataka
kuboresha Mitaala yao ili mafunzo
wanayoyatoa yaendane na wakati ikiwa ni pamoja na kukidhi mahitaji ya soko la ajira ili kuongeza fursa
ya vijana kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua maendeleo ya
ujenzi wa karakana itakayotumiwa na wanafunzi wanaosoma kozi ya ufundi uwashi
katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Manyara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.