Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo leo amewasilisha taarifa ya
tathmini ya Ubora wa elimu kutokana na Utekelezaji wa Programu ya Lipa
Kulingana na Matokeo (EP4R) kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii.
Akiwasilisha tathmini ya programu
ya EP4R kwenye Kamati hiyo ya Bunge Dkt. Akwilapo ameeleza kuwa programu imekuwa
na mafanikio tangu ilipoanza kutekelezwa mwaka 2014.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwasilisha taarifa ya tathmini ya ubora wa
Elimu kutokana na utekelezaji wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo wakati
wa kikao na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii jijini
Doodma.
Dkt. Akwilapo amesema fedha
zinazopatikana kutokana na utekelezaji wa vigezo (DLRs) katika ngazi ya
Serikali kuu na serikali za Mitaa ni kuwa fedha hizo hutumika katika kuboresha
utoaji wa elimu nchini kwa kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu
ikiwemo ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya.
Dkt. Akwilapo ameieleza kamati
hiyo ya Bunge kuwa programu ya EP4R ni ya miaka minne na inatekelezwa kwa
ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Serikali ya Sweden (SIDA) na Serikali
ya Uingereza (DFID) na kuwa mradi huo utakamilika 2020.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
kamati hiyo ya Bunge Peter Serukamba na Mbunge wa Nzega Mhe. Hussein Bashe
wameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kusimamia vizuri
utekelezaji wa mradi huo wa EP4R ambao umekuwa na matokeo chanya katika nchi.
“Katika kusimamia Programu hii ya
EP4R, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya kazi nzuri na matokeo
yanaonekana. Miundombinu imeboreka sana,” alisema Mhe. Hussein Bashe.
Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya
Jamii wakifuatilia Taarifa ya Utekelezaji wa Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo
(EP4R) Jijini Dodoma
Taarifa zinazowasilishwa kwenye
kamati hiyo ni pamoja na ile ya mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo, taarifa ya
utekelezaji wa shughuli za Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa na utekelezaji
wa shughuli za Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni,
jijini Dar es salaam.
Kikao hicho cha siku tatu
kimeanza leo na kitakamilika Novemba 1, mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.