Jumatano, 30 Januari 2019

KATIBU MKUU AKWILAPO AFUNGUA MAFUNZO ELEKEZI KWA WAAJIRIWA WAPYA NA KUWATAKA KUHESHIMU TARATIBU ZA KAZI

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amesema rasilimali watu yenye ujuzi, maarifa na utayari wa kufanya kazi ndio mtaji mkuu kwa Taasisi yoyote katika kufikia malengo yake.

Katibu Mkuu Akwilapo ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati wa kufungua mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo ambapo amewataka kutambua kuwa wana mchango mkubwa katika kuhakikisha malengo ya Wizara yanafikiwa.

“Ni vema mtambue kuwa mafanikio ya Wizara yetu na Jamii kwa ujumla yanategemea juhudi zetu kwa pamoja, hivyo mafunzo haya yakawe chachu ya nyie kupata ujuzi na maarifa utakaowasaidia kukuza kiwango cha utendaji wa kazi kwa ufanisi na kuongeza tija kwa umma,” aliongeza Dkt Akwilapo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akifungua Mafunzo Elekezi kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo jijini Dodoma ambapo amewataka watumishi hao kuheshimu taratibu za kazi ili kufikia malengo mapana ya Wizara.

Amesema utendaji uliotukuka ni ule unaofuata misingi na miiko ya kiutendaji lakini pia sheria, kanuni na taratibu na kutaka kila mtumishi kuhakikisha anaelewa taratibu hizo na kuzitumia wakati wa kutekeleza majukumu yake ya kikazi bila kumuonea mtu.

Awali Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu ya Wizara hiyo, Sebastian Inoshi alimueleza Katibu Mkuu kuwa mafunzo hayo yatafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza imeshirikisha takribani watumishi arobani na nne.
Mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya yameanza leo Januari 15, 2019 na yameshirikisha waajiriwa wapya kutoka Wizara ya Elimu Makao Makuu.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

15/01/2019 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni