Jumatano, 6 Februari 2019

KITENGO CHA MANUNUZI WIZARA YA ELIMU CHATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUFUATA SHERIA NA KANUNI ILI KUEPUKA HOJA ZA MKAGUZI MKUU

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amekitaka Kitengo cha Manunuzi na Ugavi cha Wizara hiyo kuhakikisha kinafanya kazi zake kwa kufuata sheria na kanuni za manunuzi ili kukwepa hoja za ukaguzi ambazo zimekuwa zikiripotiwa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali   (CAG).

Prof. Mdoe ametoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati wa  ufunguzi wa kikao kazi kinachowahusisha wajumbe wa bodi ya manunuzi, Idara ya   manunuzi , kitengo cha ukaguzi wa ndani  na kitengo Cha sheria kutoka Wizara hiyo  lengo likiwa ni kuimarisha Kitengo cha manunuzi kuondokana na hoja za wakaguzi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Dkt. Leonard Akwilapo, Naibu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe na Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi na  Ugavi Hirtudice Jisenge wakifuatilia mada inayotolewa wakati wa Kikao Kazi cha wajumbe wa bodi ya manunuzi, maafisa manunuzi, kitengo Cha wakaguzi wa ndani na kitengo Cha Sheria cha kuwajengea uwezo kuhusu kanuni na sheria za manunuzi.


Naibu Katibu Mkuu huyo amewaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa Kitengo hicho kimekuwa na shughuli za manunuzi ambazo zinatumia kiasi kikubwa cha fedha za serikali kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya vyuo na shule, hivyo ni muhimu kuimarisha shughuli za manunuzi ili kuokoa fedha ambazo zinaweza kupotea kwa kutofuatwa kwa taratibu.

"Wizara imekuwa na miradi mbalimbali ambayo inachukuakaribu asilimia 75 ya bajeti ya Wizara, hivyo mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo washiriki ili waweze kutoa maamuzi sahihi manunuzi, pia  kuwakumbusha wajibu wao wa kufuata sheria na kanuni za manunuzi,”amesema Profesa Mdoe.
Washiriki wa kikao kazi Cha mafunzo ya Sheria za manunuzi wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi. Kikao kazi hicho kinafanyika mkoani Morogoro.

Akizungumzia umuhimu wa kikao kazi hicho,  Mkurugenzi wa Kitengo cha Manunuzi  wa Wizara hiyo Hirtudice Jisenge amesema mafunzo hayo yatawezesha Kitengo hicho kujipanga na  kufanya kazi kwa ufanisi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni