Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha
zinaweka mikakati ya kuwamotisha walimu wapya wanaoripoti kazini kwa
kuwafikisha katika vituo vyao vya kazi ikiwa ni pamoja na kuwalipa maslahi yao
yote.
Waziri Mkuu ameyasema hayo
jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa sita wa Umoja wa Maafisa
Elimu Mikoa na Wilaya (REDEOA) na kusisitiza kuwa hatua hiyo iende sambamba na kuendelea
kuwatembelea walimu hao katika vituo vyao vya kazi kuwasikiliza, kushauriana na
kupatia ufumbuzi changamoto walizo nazo.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akifungua Mkutano Mkuu
wa sita wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya
(hawapo pichani) Jijini Dodoma.
|
Amesema walimu hao
wanaporipoti wanakuwa ni wageni katika wilaya hizo hivyo kuwaelekeza tu
kuripoti katika shule walizopangwa haitoshi ni vyema kuweka utaratibu wa kutumia
magari ya Halmashauri kuwafikisha walimu hao katika vituo vyao vipya vya kazi.
“Ninyi Maafisa Elimu
hakikisheni walimu hao wanaporipoti wanalipwa maslahi yao ya msingi, lakini pia
hamasisheni Halmashauri zenu kuwamotisha walimu kwa kuwapa vianzilishi vya
maisha kama ambavyo Wilaya nyingine zinafanya. Wilaya za Mkoa wa Njombe tangu
mwaka 2013 zimekuwa zikitoa motisha kwa walimu wapya wanaoripoti kwa kuwapa kitanda,
godoro, gunia la mahindi, viazi na maharage, hii inamfanya mwalimu kujisikia
yuko nyumbani, muige mfano huu,” aliongeza Waziri Mkuu Majaliwa.
Katika hatua nyingine Mhe.
Majaliwa amewataka Maafisa Elimu hao kutumia mkutano huo kukumbushana wajibu
wao katika kusimamia Elimu na kubadilishana uzoefu na mbinu mbalimbali za
kusimamia elimu ili kuongeza ubora wa elimu hiyo.
“Mkutano huu umekuja kipindi
muafaka kwa sababu matokeo ya upimaji wa Taifa wa ngazi mbalimbali yameshatoka,
wote tunakumbuka upimaji umefanyika kwa mitihani ya darasa la nne, la saba, kidato
cha nne na ile ya kidato cha sita, hii itoe fursa kwenu kujipima na kuona kama hatua
mliyofikia ni nzuri na kama bado ni ya chini basi mbainishe changamoto
zilizopelekea kuwa hivyo na kuweka mipango ya kuboresha,” alisema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewataka Maafisa Elimu
kusimamia Sera, Miongozo na Taratibu zinazosimamia utoaji wa elimu nchini huku
akiwasihi maafisa hao kutoa taarifa zilizo sahihi kwani wakati mwingine taarifa
zinazotolewa zinatofautiana na zile zinawasilishwa baada ya kufanyika kwa
ukaguzi katika maeneo mnayoyasimamia.
“Wakati mwingine mnatoa
taarifa zisizo sahihi, kwa sababu kaguzi ambazo zimekuwa zikifanyika zinaonesha kuna baadhi ya
maeneo ambayo bado kuna mrundikano mkubwa wa wanafunzi kati ya 73 hadi 200 kwa
upande wa sekondari na mazingira yanapokuwa katika hali hiyo si rahisi kutoa
elimu bora, hivyo tutoe taarifa zilizo sahihi na taarifa hizi zikiwa sahihi
itasaidia hata wakati wa uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza
na kile cha tano,” aliongeza Waziri Ndalichako.
Nae Mwenyekiti wa Umoja wa
Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya Germana Mng’ao ameipongeza Serikali kwa kuboresha
mazingira ya kufundishia na kujifunzia
na kuahidi kufanya kazi kwa bidii katika nafasi yao ya kusimamia Elimu
Tanzania.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni
“ELIMU BORA ITATUFIKISHA KATIKA UCHUMI WA KATI IFIKAPO 2025.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.