SERIKALI imesema iko
katika hatua za mwisho kukamilisha Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu
ambayo itatoa mwongozo wa namna ya utekelezaji wa masuala ya ubunifu na
kuwatambua wabunifu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mh. William Ole Nasha jijini Dar es
Salaam wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Ubunifu iliyoandaliwa na Mfuko wa Ubunifu
kwa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia
(COSTECH).
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. William Ole Nasha akizungumza na wabunifu (hawapo pichani) katika ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Ubunifu yanayofanyika jijini Dar es Salaam. |
Ole Nasha amesema, serikali
ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele katika teknolojia ili kuongeza chachu ya
maendeleo na ipo tayari kufadhili bunifu mbalimbali zitakazochangia maendeleo ya uchumi wa Viwanda ifikapo
2025.
Naibu Waziri Ole
Nasha amewataka waandaji wa maonesho hayo kuyapeleka katika maeneo ya wazi na
rahisi kufikika ili wananchi wengi wapate fursa ya kujionea bunifu hizo.
"Wabunifu wengi ni
wale wanaokumbana na changamoto za kila siku na kujaribu kuangalia namna ya
kuzitatua hivyo wakati mwingine mtakapoandaa wiki ya ubunifu muhakikishe kwamba
mnaweka katika maeneo ya wazi kwa ajili ya kuwakutanisha wabunifu wengi na
wananchi ili waweze kujua kinachofanyika," ameeleza.
Aidha Ole Nasha amewaasa
wabunifu kufanya bunifu zitakazoendana na changamoto za maisha zilizopo nchini
na siyo kufanya bunifu za kujifurahisha sababu wanaweza kukosa soko.
Naye, Kiongozi Mkuu wa Mfuko
(HDIF), David McGinty amesema wadau wa maendeleo nchini, wamekuwa wakichangia
Tanzania kupanda viwango vya kimataifa vya ubunifu kwani mpaka wanafunzi wa
vyuo na sekondari wanahamasishwa kutumia teknolojia kwa ajili ya kujifunzia.
Wiki ya Ubunifu
inatekelezwa na Mfuko wa Ubunifu kwa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana
na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na wadau wengine.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. William Ole Nasha na Naibu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa ubunifu. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.