Alhamisi, 14 Machi 2019

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YAKAGUA MRADI WA UPANUZI NA UKARABATI WA JENGO LA UTAWALA DUCE



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. James Mdoe wakati alipowasili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) kwa ajili ya kikao cha pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea chuo hicho kukagua utekelezaji wa Mradi wa upanuzi na ukarabati wa jengo la Utawala la chuo hicho.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeiagiza serikali kuhakikisha inafanikisha upatikanaji wa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha ukarabati na upanuzi wa jengo la Utawala la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Peter Serukamba Jijini Dar es Salaam baada ya kukagua utekelezaji wa Mradi huo wa ukarabati na upanuzi wa jengo hilo ambapo amesema kuchelewa kumalizika kwa wakati kunaweza kusababisha kuongezeka kwa gharama za ujenzi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupanda kwa gharama za vifaa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na Mwenyekiti Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba wakipitia taarifa ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa jengo la Utawala la Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Mhe. Serukamba amesema kiasi hicho cha fedha ni muhimu kikapatikana kwa sasa ambapo kazi ya ujenzi na ukarabati ikiwa inaendelea kwani itasaidia pia kuondoa usumbufu kama jengo hilo litakamilishwa nusu na kuanza kutumika.

“Kucheleweshwa kwa fedha zilizobaki zitafanya jengo hili kujengwa kwa gharama kubwa sana kwani vifaa vya ujenzi vinapanda, lakini pia haitakuwa vizuri kumalizia upande mmoja wa jengo watu waingie wafanye kazi baadaye wapishe ujenzi inakuwa ni usumbufu kwa watumishi” amesema Mhe. Serukamba.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na baadhi ya Viongozi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) wakielekea katika jengo la Utawala linalokarabatiwa.
Aidha, Mhe. Serukamba amekitaka Chuo hicho kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha maktaba ya Chuo hicho inakuwa kamilifu na kupewa kipaumbele ili kuwa na maktaba inayojitosheleza kwa kuwa na eneo lenye ubora, vitabu vya kutosha ikiwemo vitabu vya elektroniki.  Vilevile ameutaka Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuweka utaratibu wa wanafunzi wa DUCE kuweza kutumia maktaba ya kisasa iliyopo katika kampasi yake kuu

Pamoja na hayo Kamati pia imeitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimamia madai ya watumishi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ujumla na kuhakikisha madai stahiki yanalipwa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakisikiliza taarifa ya maendeleo ya kazi ya upanuzi na ukarabati wa jengo la Utawala katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).
Awali Rasi wa Duce, Prof. Bernadeta Killian ameieleza Kamati hiyo kuwa Mradi huo wa upanuzi na ukarabati jengo la Utawala unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 3.2 kwa ujumla, kiasi ambacho kinajumuisha gharama za ujenzi, ukarabati, kuweka mifumo ya TEHAMA pamoja na samani za ndani za jengo hilo ambapo mpaka sasa bado kiasi cha Shilingi Bilioni 1.1 kinahitajika ili kukamilisha.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea Mradi huo na ameahidi kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na viongozi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukagua maendeleo ya kazi ya upanuzi na ukarabati wa jengo la utawala katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni