Rais Mstaafu wa awamu Tatu Benjamin William Mkapa amekipongeza Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan JUCo kwa
kutimiza jubilee ya miaka 25 ya utoaji huduma ya Elimu ya Juu nchini na
kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa Chuo hicho na vyuo vingine binafsi
katika kuwezesha upatikanaji wa elimu nchini hususan elimu ya juu .
Mhe. Mkapa amesema hayo katika
kilele cha sherehe za Jubilee zilizofanyika katika Chuo hicho jijini
Morogoro na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Aidha
amesema pamoja na kazi nzuri wanayofanya vyuo binafsi, ada zinazotozwa katika
vyuo hivyo bado ziko juu, hivyo amevitaka kuhahakisha wanajiendesha kwa gharama
nafuu bila kuathiri ubora na kuhakikisha wanatoza ada kwa viwango ambavyo Watanzania walio wengi watamudu na kuweza kupata elimu hiyo kwa maendelo yao na
taifa kwa ujumla.
“Niseme kuwa Elimu pekee ndiyo
inachangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na baadae Taifa kwa ujumla, hivyo ni
vyema gharama za ada ziwe ni zile ambazo wananchi wa kawaida watamudu, ikumbukwe
kuwa wananchi walio wengi wanategemea mikopo inayotolewa na Serikali, sasa Vyuo
binafsi ni vyema vikaliangalia hili,” alisema Mzee Mkapa.
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa akiwa
ameongozana na viongozi mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25
ya Chuo Kikuu Cha Jordan kilichopo Mkoani Morogoro.
Awali akizungumza katika Jubilee
hiyo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema
Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu ya juu ili kuongeza
ubora na kuwa haitavifumbia macho vyuo ambavyo havitatii na kuzingatia
vigezo, sheria, taratibu na kanuni za uendeshaji wa vyuo hapa nchini.
“Nitoe wito kwa vyuo vyote
nchini kuhakikisha vinakidhi vigezo vya uendeshaji wa vyuo, tofauti na hapo
serikali haitasita kuchukua hatua stahiki kwa vyuo vitakavyokwenda kinyume.
Lengo la serikali ni kuhakikisha Elimu bora inatolewa nchini ili kuzalisha
wataalamu wenye uwezo na maarifa kwa ukuaji wa uchumi,”alisema Waziri
Ndalichako.
Waziri Ndalichako amesema hadi
sasa Tanzania kuna vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 49 ambapo kati ya
hivyo 34 ni vyuo binafsi ambayo ni sawa na asilimia 69.4, hivyo Serikali
inatambua mchango mkubwa wa Vyuo binafsi na amekipongeza Chuo Cha Jordan kwa
kutimiza miaka 25.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William
Mkapa akizindua Kitabu Maalumu wakati wa maadhimisho ya kutimiza miaka 25 kwa
Chuo Kikuu Cha Jordan, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia pia alishiriki
maadhimisho hayo.
Aidha Waziri Ndalichako
alisisitiza pia kuwa serikali inaendelea kuimarisha Bodi ya Mikopo ili kutoa
mikopo zaidi kwa wanafunzi ambapo alisema kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hiyo ambapo kutoka mwaka 2004/05 hadi
mwaka 2018/19 wanufaika wa mikopo kwa ujumla ni 480,405.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe amesema Chuo Cha Jordan kutimiza miaka
25 ni hatua kubwa na kuwa Chuo hicho ni miongoni mwa vyuo vya mfano katika mkoa
huo kwa sababu mkoa haujawahi kupokea taarifa za wanafunzi wa Chuo hicho
kujihusisha na makundi wala vitendo viovu. Aidha ameahidi kushirikiana na chuo
hicho kwa kutumia watalaamu wanaoandaliwa hapo kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa.
Baadhi ya Wanafunzi na wageni mbalimbali
wakifuatilia hotuba mbalimbali za Viongozi wakati wa Maadhimisho ya Miaka 25 ya
Chuo Kikuu cha Jordan kilichopo Mkoani Morogoro.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.