Alhamisi, 7 Machi 2019

OLE NASHA AMUAGIZA KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU KUFUATILIA UKARABATI SHULE YA SEKONDARI KIBAHA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Leornald Akwilapo kufika katika shule ya Sekondari Kibaha kujionea jinsi kazi ya ukarabati ilivyo chini ya kiwango ili achukue hatua zinazostahili.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo alipofanya ziara katika shule ya sekondari Kibaha kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika shule hiyo.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya Sekondari Kwala iliyopo katika Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani yanayojengwa na wizara kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) 
Kiongozi huyo amesema hajaridhishwa kazi  inavyoendelea kwani hailingani na fedha ambayo tayari imeshalipwa na serikali tangu mwaka juzi walipokabidhiwa. Kazi  hii ya ya ukarabati wa jingo la bweni na jingo la maabara ya fizikia katika shule hiyo inayotekelezwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA).

“Wakala huyu alipaswa kuwa amekamilisha ukarabati na ujenzi wa miundombinu jumla 31 katika shule hii, lakini mpaka sasa amekarabati majengo mawili tu na ukiyaangalia  yako chini ya viwango huku akiwa ametumia zaidi ya kiasi cha shilingi milioni 400,” Amesema Ole Nasha.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua vifaa vya ujenzi wa mabweni katika shule ya Sekondari Kwala iliyopo katika Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani baada ya kutoridhishwa na taarifa ya ujenzi iliyotolewa kwake na Mkuu wa shule hiyo kuhusu vifaa vilivyotumika katika mradi huo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri amewapongeza wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa bila kujali changamoto walizonazo za miundombinu ya mabweni, madarasa pamoja na vyoo.

“Wanafunzi hawa wanachukua mchepuo wa sayansi wanahitaji kujiongezea maarifa sasa nimeambiwa shule hii ina kompyuta nne tu hivyo namuagiza Katibu Mkuu alete kompyuta 50 shuleni hapa ziweze kuwasaidia wanafunzi” alisisitiza Naibu Waziri

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akijadiliana na baadhi ya walimu na wajenzi katika shule ya sekondari ya Kwala ambapo wizara inatekeleza mradi wa ujenzi wa mabweni mawili kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo.
Kwa upande wake Kaka Mkuu wa Shule hiyo Jonas Baraka amemweleza Naibu Waziri kuwa wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi za miundombinu kwani hata ile iliyokarabatiwa kwani vyoo havipitishi maji, ubovu wa vitasa vya milango pamoja na ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo ya shule.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na wazazi, wanafunzi, walimu pamoja na wanakijiji wa Kwala mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya Sekondari Kwala na kuwata wanakijiji hao kuchangia katika mradi huo ili ukamilike mapema.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri ameonyeshwa kutoridhishwa na matumizi ya zaidi ya shilingili milioni mia moja na hamsini ziliotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika sekondari ya Kwala na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Asumpter Mshama kutuma vyombo vya ulinzi na usalama kwenda kukagua mchakato mzima uliotumika katika ujenzi wa mabweni mawili ya shule hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akitembelea maeneo mbalimbali ya shule ya sekondari Kibaha akiwa ameambatana na Mbunge wa Kibaha Mjini Mhe. Silyvestry Koka na wanafunzi wa shule hiyo.
Naibu Waziri Ole Nasha yupo katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule inayofadhiliwa na Wizara ya Elimu kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika Mkoa wa Pwani katika wilaya za Kibaha, Kisarawe na Rufiji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni