Jumatano, 6 Machi 2019

SERIKALI YATOA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI MOJA KUJENGA NA KUKAMILISHA MIUNDOMBINU YA SHULE WILAYANI BUHIGWE-KIGOMA


Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga na kukamilisha miundombinu ya shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa ulioanzishwa kwa nguvu za wananchi katika shule ya sekondari Janda iliyopo katika kata ya Janda wilayani Buhigwe.
Waziri waElimu, SayansinaTeknolojiaProfesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya nyumba za walimu ambazo katika shule ya Sekondari Janda iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma.
Waziri Ndalichako pamoja na kupongeza hatua hiyo ya wananchi amesema tayari Wizara kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo(EP4R) imeingiza fedha zaidi ya shilingi milioni Mia Tisa   kwenye akaunti ya Halmashauri ya Buhigwe ambazo zitatumika kuanza ujenzi wa shule mpya ya msingi yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 945 na kundeleza ujenzi wa miradi mingine ya shule ambayo haijakamilika.

 “Kwanza niwapongeze wananchi wa Buhigwe kwa hatua hii, hapa  kwenye Halmashauri ya Buhigwe bado kuna kazi kubwa ya kufanya, ukiangalia idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na idadi ya sekondari zilizopo, bado wanafunzi wengi  wanabaki hivyo nawasihi wananchi endeleeni kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule na serikali itaunga mkono juhudi hizo”, alisema Waziri Ndalichako.
Waziri waElimu, SayansinaTeknolojiaProfesa Joyce Ndalichako akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari Janda iliyoko Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu na kufikia malengo yao.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameeleza kusikitishwa na ufaulu duni wa wanafunzi wa kike katika mkoa wa kigoma na hasa  shule ya sekondari  Janda na kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii.

“Nimeangalia  katika matokeo yenu miaka miwili iliyopita hakuna anaepata daraja la kwanza, mnaanzia daraja la tatu hadi sifuri kwa nini hamjitahidi, serikali inalipa ada  ili ninyi msome nahitaji mabadiliko ongezeni juhudi katika masomo,” aliongeza waziri Ndalichako.
Muonekano wa Hatua ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule ya Sekondari Janda iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Mkoani Kigoma.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Luteni Kanali Michael Ngayalina alimweleza Waziri kuwa Halmashauri hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa 25, na kusema kuwa tayari ameagiza kila kijiji kujenga darasa moja katika shule ya kata.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.