Jumapili, 3 Machi 2019

WAZIRI NDALICHAKO AWATAKA WATOTO WA KIKE KUSHIRIKI MICHEZO ILI KUEPUKA VISHAWISHI


Wanafunzi wa kike nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika michezo ili kuimarisha afya ya akili katika masomo na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuharibu ndoto zao.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako  wakati wa bonanza la mpira wa miguu maarufu kama MIRIAM CUP lililoshirikisha wanafunzi wa kike kutoka shule za msingi, secondari, vyuo vya ualimu na vile vya Maendeleo ya wananchi lililofanyika wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikabidhi kombe wa wanachuo wa Chuo cha Ualimu Kasulu kilichopo Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma baada ya kuibuka kidedea katika mechi zilizoshindanisha wanafunzi wa kike kutoka shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ualimu na vile vya Maendeleo ya wananchi vilivyopo katika Halmashauri ya Kasulu.

Waziri Ndalichako amesema  lengo la bonanza hilo ni kutoa hamasa kwa watoto wa kike kujiepusha na mimba za utotoni  na kuwa michezo ikitumika vizuri ina nafasi kubwa ya kumkomboa mtoto wa kike kielimu.

'' Michezo inachangamsha akili, michezo inajenga afya iliyobora lakini pia michezo ni ajira na inaondoa vishawishi,” alisisitiza Waziri Ndalichako.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akisalimiana na wanafunzi wa kike ambao wameshiriki bonanza la mpira wa miguu almaarufu MIRIAM CUP lililoandaliwa na mdau wa Elimu Miriam Ntakisivya kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi wa kike kukataa mimba za utotoni na kuendelea na masomo.

 Waziri Ndalichako amempongeza muandaaji wa bonanza hilo ambaye ni Mdau wa Elimu Miriam Ntakisivya na kusema kuwa bonanza hilo liwe endelevu ili kuleta hamasa kwa wanafunzi wa kike mkoani Kigoma kufanya vizuri katika masomo na kupunguza mimba za utotoni.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange amesema wilaya hiyo kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2016 kumekuwa na ufaulu mdogo kwa wanafunzi wa kike wanaomaliza kidato cha nne, hivyo bonanza hilo limewaleta pamoja wazazi, walimu na jumuiya nzima ya Kasulukwa lengo la kukumbushana umuhimu wa kuwapa nafasi watotowa kike kwenye masomo.


Wanafunzi wa kike walioshiriki bonanza la mpira wa miguu wakicheza mpira katika kiwanja cha mpira kilichopo Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.

Naye muandaaji wa Bonanza hilo Miriam Ntakisivya amesema ameamua kuanzisha bonanza hilo baada ya kuona watoto wa kike mkoani humo  wanashawishiwa na vitu vidogo na kuacha shule wakiwa na umri mdogo na hivyo kuamua kuwaleta pamoja kukataa vitendo hivyo kupitia michezo.

Bonanza hilo limeshirikisha timu za wasichana nane kutoka wilaya ya Kasulu na mechi kubwa iliyohusisha  timu za watani wa jadi Kasulu United FC na Bodaboda FC.



Muandaaji wa Bonanza la mpira wa miguu kwa wanafunzi wa kike katika wilaya ya Kasulu Miriam Ntakisivya akimpa cheti cha shukrani Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.