Jumapili, 31 Machi 2019

WIZARA YA ELIMU KUJENGA MAABARA YA FIZIKIA KATIKA SHULE MAALUM YA WASICHANA KISARAWE


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  kujenga maabara ya Fizikia  katika shule mpya maalum ya wasichana inayotarajiwa kujengwa katika wilaya ya Kisarawe.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uchangiaji fedha kwa ajili ya kujenga shule hiyo ambapo Waziri Ndalichako amesema pamoja na kujenga Maabara pia itatoa vifaa vyote vya maabara hiyo lengo likiwa kuhamasisha na kuongeza fursa za watoto wa kike kisarawe na kwingine nchini kusoma masomo ya sayansi.

Akizungumzia hafla ya kuchangia fedha kwa ajili ya kujenga shule hiyo maalum Waziri Ndalichako ameipongeza wilaya ya Kisarawe kwa kuja na kampeni ya Tokomeza Zero yenye lengo la kuboresha elimu katika wilaya hiyo huku mkazo ukiwekwa katika  kumuondolea mtoto wa kike changamoto anazokabiliana nazo wakati wa kujifunza kwa kuhakikisha anapata mazingira rafiki na salama ya kujifunzia.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza na wadau mbalimbali wa elimu (hawapo pichani) walioitikiwa wito wa kuchangia ujenzi wa shule maalum kwa ajili ya watoto wa kike katika Wilaya ya Kisarawe



“Mtoto wa kike anapokuwa anatembea umbali mrefu kutoka shuleni kwenda nyumbani njiani anakutana na majaribu na vishawishi vingi vinavyokwamisha lengo lake la kupata elimu, kwa hiyo kuamua kujenga shule maalum kwa ajili ya mtoto wa kike ni uamuzi mzuri kwani  itawapa fursa kuweza kukaa na kusoma vizuri zaidi na hii ni hatua kubwa sana katika kuunga mkono Jitihada zinazofanywa na Rais wetu” Amesema Ndalichako.

Ndalichako amesemea  tathimini inaonyesha ufaulu kwa ujumla kwa mtoto wa kike uko chini ukilinganisha na watoto wa kiume kwa hiyo ujio wa shule hii maalum kwa ajili ya mtoto wa kike ni muhimu kutokana na mazingira wanayoishi ambapo wanaporudi kutoka shule wanakuwa na majukumu mengi ya nyumbani na kuwanyima muda wa kujisomea.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo amesema wilaya ya Kisarawe imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inapunguza ziro na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikikwamisha wanafunzi kujifunza hasa kwa mtoto wa kike.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako, Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti maalum wa Kisarawe Zainabu Vulu wakifatilia kwa makini zoezi la  wa kuchangia ujenzi wa shule maalum kwa ajili ya watoto wa kike katika Wilaya ya Kisarawe

“Wilaya ya Kisarawe imekuwa na utaratibu wa kufanya tathimini kila matokeo yanapotoka ili kuona nafasi ya wilaya katika ufaulu na kuziangalia changamoto ambazo zinakwamisha faulu na kuziwekea mikakati ili kuboresha mazingira ya kfundishia na kujifunza ” amesema Waziri Jafo.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Joketi Mwegelo alimweleza Waziri wa Elimu kuwa lengo la kuanzishwa kwa Kampeni ya Tokomeza Zero ni kuongeza na kuboresha miundombinu ya shule ili kuifanya kuwa rafiki na salama kwa utoaji wa elimu.

Mwegelo amesema ujenzi wa shule maalum katika wilaya ya kisarawe  ya uchangia ni moja ya mkakati mahsusi wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto wa kike ili kuwawezesha kupata muda wa ziada wa kujifunza zaidi.

Shule ya Sekondari maalum inayotarajiwa kujengwa katika wilaya Kisarawe itachukua wanafunzia wa kidato cha kwanza mpaka cha sita na inakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na nusu ambazo zinahusisha ujenzi wa miundombinu ya mabweni, madarasa, maabara, matundu ya vyoo pamoja na nyumba za walimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako na  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo kwa pamoja wakipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni kmi iliyolewa na kampuni ya star times kwa ajili ya ujenzi wa wa shule maalum kwa ajili ya watoto wa kike katika Wilaya ya Kisarawe

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni