Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako
amezindua ukumbi wa mihadhara wa kisasa katika Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
uliojengwa mapato ya ndani ya Chuo hicho.
Akizundua ukumbi huo wa Mihadhara kigamboni jijini Dar es
salaam Waziri Ndalichako amepongeza Bodi ya Utawala na Uongozi wa Chuo hicho kwa
kusimamia vema matumizi ya fedha zinazotokana na Mapato ya ndani na kutumia kutekeleza
miradi yenye tija kwa Chuo na Taifa kama ilivyofanyika katika ujenzi wa Ukumbi huo
na pia amewataka uongozi kusimamia Dira na Dhima ya uanzishwaji wake kwa kujikita
katika kutoa mafunzo ya Uongozi, Utawala na Maadili.
Waziri Ndalichako amewapongeza Watendaji wa Chuo kwa kusimamia
kwa karibu utekelezaji wa Mradi huo hadi kufikia hatua ya kukamilisha japo kwa kuchelewa
kwa karibu miezi tisa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Ukumbi mpya wa Mihadhara
uliyojengwa katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Kivukoni uliojengwa
kwa kutumia mapato ya ndani ya Chuo hicho.
“ nimefurahishwa na kazi hii nzuri iliyofanyika hapa, kwakweli
ni jengo zuri lenye ubora wa hali ya juu na ambalo litawafanya wanafunzi kuongeza
ari ya kujifunza na ninategemea kuona jengo hili likituzwa vizuri ili litumike kwa
miaka mingi likiwa na ubora uleule”. Amesisitiza Ndalichako
Aidha Ndalichako amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuthamini na kutumia vizuri mapato yake ya ndani
kwa ajili ya kutekeleza mipango na Miradi mbalimbali ya Maendeleo katika taasisi
hizo ili kuleta maendeleo ya haraka badala ya kuzitumia fedha hizo kwa matumizi
mengine yasiyo na tija.
Wakati huo amewataka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao
ni wakandarasi wa ujenzi wa Ukumbi huo kukamilisha
miradi mingine iliyo chini ya Wizara ya Elimu ikiwemo ukarabati wa shule Kongwe
mfano Kibaha Sekondari, Shule ya Sekondari ya Wasichana Songea pamoja na ujenzi
wa Hosteli na miundombinu mingine katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili Kampasi ya Mloganzila.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Utawala ya Chuo hicho Stephen Wasira,
amesema Chuo hicho kimejipanga kuhahakisha kinatoa elimu bora na wahitimu walio
bora wenye weledi hasa katika eneo la uongozi na utawala ili kuenzi fikra na maono
ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alieanzisha chuo hicho Mwaka 1961
kwa lengo la kuandaa viongozi na watawala.
Awali, Mkuu wa Chuo Prof. Shadrack Mwakalila akitoa taarifa
ya mradi amesema jengo hilo limegharimu zaidi ya Shilingi za Tanzania Bilioni 1.1 na kwamba lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 330
kwa wakati mmoja. Ameongeza kuwa pamoja na ukumbi wa Mihadhara jengo hilo lina ofisi
nane za wahadhiri na mifumo ya kisasa ya sauti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.