Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi za Serikali
na zisizo za Serikali ambazo zinajihusisha na masuala ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano(TEHAMA) kuibua vipaji vya wanafunzi na kuviendeleza.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati
wa hafla ya kufunga mafunzo na mashindano ya kitaifa ya wasichana na Tehama yaliyoandaliwa
na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Jijini Dodoma.
Waziri
Ndalichako amesema ni vyema vipaji vya wanafunzi washiriki wa mafunzo na mashindano
ambavyo vimeibuliwa vikaendelezwa kwa kuwa vinalenga kutumia TEHAMA kutatua changamoto
zilizopo katika jamii yetu na kusisitiza kuwa Serikali inahimiza matumizi sahihi
ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa maendeleo ya Taifa.
Kiongozi
huyo ameipongeza UCSAF kwa kuandaa mafunzo na mashindano hayo kwa wanafunzi wa
kike kutoka shule mbalimbali za umma nchini, ambapo pia amesisitiza kuwa vijana
wote wa kike na wa kiume wana vipaji na ni wabunifu wanachohitaji ni vipaji vyao
kuibuliwa kwa kupewa fursa na kuendelezwa.
“Niwasihi
sana wadau wote, vijana na hususan wanafunzi kuhakikisha mnatumia vema teknolojia
ya habari na mawasiliano kwa sababu inaweza kuwakuza kitaaluma, kiuchumi na kijamii
kwa ujumla wake kama ikitumika vizuri,” alisema Waziri Ndalichako.
Amesema
nia ya serikali ni kuona mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu unaongeza tija
katika uzalishaji hususan katika sekta ambazo zinagusa wananchi walio wengi ikiwemo
kilimo, mifugo, viwanda pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma katika
jamii.
“Mnaweza
kuona hapa wanafunzi wa kike wametengeneza application ya kutoa huduma kwa mama
mjamzito na hayo ni mafunzo ya siku nne tu, je wangeongezewa muda? Hii inaonesha
watoto wa kike wanaweza,“ aliongeza Waziri Ndalichako.
Aidha
Waziri Ndalichako amewataka watanzania hususan vijana kutumia teknolojia ya habari
na Mawasiliano kwenye shughuli za kimaendeleo badala ya kujikita katika mitandao
ya kijamii ya facebook na instagram huku akiwaasa wanafunzi kutumia Tehama
katika masuala yanayoleta tija badala ya kutumia muda mwingi kuchat vitu visivyo
na tija.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo
na mashindano ya kitaifa ya wasichana na TEHAMA wakifuatilia hotuba ya Waziri
wa elimu.
|
Naye Mtendaji Mkuu wa
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter Ulanga amesema Mfuko huo katika mikakati yake imejipanga kuhakikisha
inafikisha elimu ya TEHAMA pamoja na kutoa vifaa kwa shule za umma hapa nchini na
kwamba hadi sasa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umekwisha peleka kompyuta katika
shule za umma 500 ambapo kila shule imepata kompyuta 5 ikiwa ni pamoja na kutoa
mafunzo ya TEHAMA kwa walimu zaidi ya 500.
Mhandisi Ulanga, alieleza kuwa mafunzo na mashindano
hayo ni sehemu ya maadhimisho ya kimataifa ya siku ya MTOTO WA KIKE na TEHAMA
Duniani yanayoadhimishwa mwezi Aprili kila Mwaka na kuhusisha wanafunzi wa kike
toka mataifa mbalimbali. Maadhimisho hayo yaliyoambatana na mafunzo ya siku nne
yalikuwa na Kaulimbiu isemayo ‘Kuongeza mipaka na kubadili mitizamo’ na yameshirikisha wanafunzi
wa kike zaidi ya 240 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambapo wanafunzi
6 kati yao wameibuka washindi na kuzawadiwa vikombe pamoja na kompyuta na fursa
ya kushiriki katika Maadhimisho ya kimataifa yatakayofanyika nchini Ethiopia.
Ulanga aliongezea kuwa
UCSAF itaendelea na mpango huo na kuongeza idadi ya washiriki ili kukuza ujuzi na
kuhamasisha matumizi sahihi ya TEHAMA miongoni mwa wanafunzi wa kike nchini na kuwashukuru
wadau wote walioshiriki kufanikisha maadhimisho hayo mwaka huu, ikiwemo,
Vodacom, DIT, UDOM, CBA Bank na TERMET.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.