Jumapili, 14 Aprili 2019

HESLB SASA YATOA ELIMU UOMBAJI MIKOPO SHULENI

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanza kuendesha programu za elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari waliopo mikoani ili kuwaelimisha kuhusu sifa na taratibu za kuomba mikopo kwa usahihi.

Akizungumza wilayani Maswa, mkoani Simiyu na wanafunzi 1,166 wa kidato cha sita kutoka shule zote 12 za mkoa huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema uendeshaji wa programu hizo unalenga kuondokana na changamoto wanazopata wanafunzi wakati wa kuomba mikopo ya elimu ya juu. HESLB ilianza kuendesha programu hizo katika mkoa wa Dar es Salaam.

Wanafunzi hao wapo katika kambi iliyoandaliwa na uongozi wa mkoa wa Simiyu kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya kidato cha sita inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao wa Mei. Kambi hiyo ipo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu Dkt. Seif Shekalaghe akiongea katika mkutano kati ya HESLB na wanafunzi 1,166 wa kidato cha sita kutoka mkoa wa Simiyu. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru. HESLB inaendesha programu za elimu ya uombaji mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa kidato cha sita nchini kote.
“Uzoefu wetu na maoni ya wadau wetu umetufanya tuanzishe programu hizi nchini kote ili wakati wa kuomba mikopo, muombe kwa usahihi na wale wenye sifa wapate na hatimaye kutimiza ndoto zao,” aliwaambia wanafunzi hao na kueleza kuwa kuanzia kesho (Aprili 15, 2019) maafisa wa HESLB watakua katika shule mbalimbali mikoani kutoa elimu hiyo.

Katika mikutano hiyo, wanafunzi wanaelezwa kuhusu sifa, nyaraka muhimu zinazotakiwa, namna ya kuomba na kuwasilisha kwa usahihi kwa njia ya mtandao na utaratibu na umuhimu wa kurejesha mkopo mara wamalizapo masomo. Katika programu hizi, wanafunzi pia hupata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi.
Mwanafunzi Casto Nyakalungu wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Binza, mkoani Simiyu akiuliza katika mkutano kati ya wanafunzi wa kidato cha sita kutoka shule 12 za mkoani humo na maafisa wa HESLB waliofika kutoa elimu kuhusu sifa na utaratibu wa kuomba mkopo.
Kwa mujibu wa Badru, katika mwaka wa masomo 2018/2019, kati ya waombaji wa mikopo zaidi ya 57,000 ambao walipata udahili vyuoni, maombi zaidi ya 9,000 yalikua na upungufu mkubwa ikiwemo kukosa nyaraka kama vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho sahihi vya wadhamini, kutosainiwa na waombaji, wadhamini au serikali za mitaa au vijiji.

Akizungumza na wanafunzi hao, Afisa Mikopo Mwandamizi kutoka HESLB Daudi Elisha aliwasihi wanafunzi hao kusoma kwa makini mwongozo utakaotolewa na HESLB mwezi ujao ambao utaeleza hatua kwa hatua kuhusu uombaji wa mkopo.

“Kuna baadhi ya waombaji wa mikopo huwa na haraka, mwezi ujao tukianza kupokea maombi, tutatoa mwongozo kwa lugha ya kiswahili na kiingereza, ninawasihi mtulie na msome kwa makini, msiwe na haraka kwa kuwa mtakuwa na miezi zaidi ya miwli ya kuomba,” alisema Elisha na kuongeza:
Afisa Mikopo Mwandamizi wa HESLB Daudi Elisha akiongea wilayani Maswa jana  na wanafunzi wa kidato cha sita kutoka shule za mkoa wa Simiyu kuhusu sifa na utaratibu wa kuomba mikopo ya elimu ya juu.
“Hivi vipeperushi tunavyowapa vina maswali na majibu 21 ambayo nayo yanawaeleza hatua kwa hatua, mkisoma na kuzingatia, naamini wale wenye sifa watafanikiwa,” alisema Elisha.

Akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dkt. Seif Shekalaghe aliishukuru HESLB kwa kutambua changamoto wanazokutana nazo wanafunzi na kuamua kuzitatua.

“Sisi kama mkoa, tunawashukuru sana kwa kuwa jitihada zetu za kuongeza ufaulu hazitakua na faida kubwa kama vijana masikini watafaulu halafu wakashindwa kutimiza ndoto zao kwa kukosa mkopo … hii ni programu nzuri sana,” amesema Dkt. Shekalaghe.

HESLB ilianzishwa mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai 2005 ili kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi watanzania wasio na uwezo na pia kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na Serikali tangu mwaka 1994/1995.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni