Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe leo
amefungua Kikao Kazi cha kupitia na kutoa maoni yatakayowezesha kuboresha
rasimu ya Mwongozo na Mpango wa Utekelezaji wa kuanzisha vituo vya Teknolojia
nchini.
Akizungumza
na washiriki wa kikao hicho mkoani Dodoma Prof. Mdoe ameainisha kuwa Mpango wa
Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, unalenga katika kujenga uchumi wa
viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu.
Amesema
Mpango huo, umebainisha umuhimu wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika
maendeleo ya nchi na Uendelezaji wa Teknolojia na Ubunifu kuwa unakabiliwa na
changamoto ya kuwepo kwa vituo mahiri vya kuzilea, kuziendeleza au kuhawilisha
teknolojia na bunifu ili kuzigeuza na kuwa fursa za kiuchumi.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia Hotuba ya mgeni
rasmi wakati wa kikao cha kujadili rasimu ya Mwongozo wa kitaifa wa kuanzisha
na kuendeleza vituo vya Teknolojia na ubunifu.
|
Prof.
Mdoe amesema vituo vya kuendeleza teknolojia na ubunifu ni nyezo muhimu katika
maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na huchochea kuwepo kwa tija katika
kuleta maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla.
“Uwepo
wa vituo hivyo hujenga mazingira wezeshi kwa Taasisi za utafiti na maendeleo
kwa kutoa huduma za kulea, kuendeleza na kuhawilisha teknolojia kwa makampuni madogo na ya kati (SMEs). Aidha, vituo hivi vina umuhimu wa kutoa ufumbuzi
wa kisayansi, na kiteknolojia katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii,”
alisisitiza Prof. Mdoe.
Washiriki wa kikao cha
kujadili rasimu ya mwongozo wa kitaifa wa kuanzisha na kuendeleza vituo vya
Teknolojia na ubunifu wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi.
|
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Prof.
Maulilio Kipanyula ameeleza kuwa umuhimu wa vituo hivyo ni kuimarisha matumizi chanya
ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kama vile Teknolojia za kuendeleza viwanda.
Kikao
kazi hicho cha siku moja kimehudhuriwa na washiriki kutoka Wizara mbalimbali,
Taasisi zinazojishughulisha na masuala ya utafiti, na Taasisi zilizo chini ya
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.