Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemuagiza Kamishna wa
Elimu kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 mafunzo ya ufundi yanaanza kutolewa kikamilifu
katika shule saba za ufundi ambazo Serikali imezikarabati.
Pia
amemuagiza kuhakikisha ifikapo
2020 michepuo inayoendana na mwelekeo wa Serikali kama kilimo
inaanza kufundishwa lakini pia kuwepo na somo la Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano kwa tahasusi za wanafunzi wa kidato cha tano.
Waziri
Ndalichako ametoa maagizo hayo mkoani Morogoro wakati wa kufunga Wiki ya
Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine ambapo amesema tukitaka watoto wetu
waweze kuingia katika soko la ushindani hatuwezi kuacha nyuma masomo hayo.
Profesa
Ndalichako aliongeza kuwa Serikali imetumia takribani shilingi bilioni moja
kukarabati shule hizo za ufundi na kwamba ni vyema zikaanza kutoa mafunzo kwa
wanafunzi ili nchi iweze kuneemeka na matunda ya utaalamu wa wanafunzi hao
pindi watakapomaliza.
Katika
hatua nyingine Waziri Ndalichako ameeleza kufurahishwa na namna Chuo Kikuu cha
Sokoine kinavyoendelea kumuenzi na kumpa heshima kubwa Hayati Edward Moringe
Sokoine ambaye alikuwa shujaa, mchapakazi, mzalendo na mtu ambaye alijitoa
katika kulitumikia Taifa na kwamba mpaka mauti yanamkuta alikuwa kazini.
“Tuna
wajibu wa kuyaishi mazuri ambayo yamefanywa na kiongozi huyu, SUA nafurahi kuona
mnawashirikisha wanafunzi katika midahalo hii ni vizuri wakajua Taifa limetoka
wapi, nchi hii imetulia kwa kuwa kuna watu walifanya kazi usiku na mchana ya
kujenga amani, umoja na mshikamano ni rahisi sana kufanya kitu kimoja cha
kuvuruga amani na mshikamano lakini ikivurugika kuijenga inaweza kuchukua karne
kuirudisha kwa hiyo tuendelee kuwaenzi waasisi wa Taifa hili kwa kuyaishi
waliyoyafanya,” alieleza Waziri
Ndalichako.
Amesema
Serikali ya Awamu ya Tano inatambua kuwa asilimia kubwa ya Watanzania ajira zao
ni kilimo na katika kuenzi mazuri yaliyofanywa na Hayati Edward Moringe Sokoine
Serikali imeendelea kukiimarisha Chuo kikuu cha Sokoine ikitambua kilimo bora
kinatakiwa kuwa na utaalamu bora.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiangalia shamba darasa la zao la zabibu
lililopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine mkoani Morogoro.
|
Kufuatia
umuhimu huo Serikali imetumia zaidi ya bilioni 2 kujenga na kununua vifaa vya maabara
ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Sokoine yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400,
pia katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali imetoa fedha zaidi ya shilingi
billioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa maabara mtambuka pamoja na bweni la wanafunzi
lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 700 pindi litakapokamilika.
Pia
kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia Chuo kimepatiwa shilingi milioni 400 kwa
ajili ya kuboresha maabara ya udongo itakayowasaidia wakulima kujua aina ya
udongo na mazao yanayostahili kupandwa kwani wakati mwingine mazao yanaweza
yasiwe na tija kwa sababu wakulima wanajipandia bila ya kuwa na utaalamu wa
kujua afya ya udongo na kile kinachostawi na kupelekea kuathiri uzalishaji.
Wakizungumzia
utendaji wa Hayati Edward Moringe Sokoine wakati wa uhai wake baadhi ya viongozi
waliowahi kufanya nae kazi akiwemo Mhe. Getrude Mongela na Mzee Paul Kimiti walisema
Kiongozi huyo alikuwa mchapakazi, muadilifu na mzalendo aliyetumia muda wake
kuipigania nchi yake bila kuchoka.
Muonekano wa shamba darasa
la zao la zabibu lililopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine mkoani Morogoro.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.