Serikali kupitia
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeahidi kutumia kiasi cha zaidi ya
shilingi milioni 700 kufanya ukarabati mkubwa wa karakana mbalimbali hasa zile
za ndaki ya kilimo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo
mkoani Morogoro.
Ahadi hiyo imetolewa na Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi wa wiki ya Kumbukizi
ya kifo cha Hayati Edward Moringe Sokoine iliyofanyika SUA Mkoani Morogoro
ambapo amesema lengo la kuzifanyia ukarabati karakana hizo ni kuziboresha ili ziendane na mwenye
jina na kuboresha utendaji kazi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akitembela shamba darasa la
mazao ya papai na nanasi katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Mkoani
Morogoro.
Dkt. Akwilapo alisisitiza kuwa
Hayati Edward Moringe Sokoine katika utumishi wake kama Waziri Mkuu wa Tanzania
aliongoza nchi kwa moyo wa uwajibikaji, kufuata sheria huku akitanguliza
uzalendo mbele kwa ajili ya nchi yake hivyo ni vizuri kutafakari mawazo ya Hayati Sokoine ambayo
yalichangia katika kujenga msingi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na
kuyaenzi kwa vitendo.
“Leo imetimu miaka 35 tangu
tulipompoteza mtoto wa kweli wa ardhi yetu, katika maadhimisho ya kifo chake
tutafakari mawazo yake ambayo yalichangia kujenga msingi kwa ajili ya maendeleo
ya kiuchumi nchini,” alisema Dkt. Akwilapo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiangalia samani
zilizotengenezwa kwa kutumia miti ya mianzi wakati akitembelea mabanda ya
maonesho katika viwanja vya SUA Mkoani Morogoro
Miongoni mwa mambo ambayo
Hayati Edward Moringe Sokoine ambaye Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimepewa
jina lake aliyapa msisitizo katika kuliletea Taifa maendeleo ni pamoja na
uzalishaji na maendeleo ya viwanda katika kilimo.
Nae
Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda amesema maonesho ya wanasayansi
na wabunifu ni sehemu ya kumuenzi Hayati Moringe Sokoine kwa kuendeleza mambo
mazuri aliyoyafanya kwa maendeleo ya Tanzania na kufanya maono yake kuwa hai kwa
ajili ya maendeleo ya Taifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiangalia shamba kisasa la
samaki na mbogamboga alipotembelea mabanda ya maonesho SUA wakati wa
maadhimisho ya wiki ya Hayati Edward Moringe Sokoine.
Profesa Chibunda aliongeza kuwa
kumbukizi hiyo kwa mwaka huu imechagizwa na maonesho hayo yanayolenga kukuza
uzalishaji katika kilimo na viwanda nchini kama ilivyoainishwa katika Programu
ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo awamu ya II (2015/16-2024/25) na Mpango wa
Maendeleo wa miaka mitano awamu ya II, (2016/17-2020/21).
Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe
Sokoine ya mwaka huu imechagizwa na mada juu ya Uzalishaji wa Viwanda kwa
Maendeleo ya Tanzania: Mambo ya kujifunza kutoka kwa Hayati Edward Moringe Sokoine na Matarajio ya
siku zijazo.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
kimekuwa kikiandaa kumbukizi ya kifo chake tangu mwaka 1992 ikihusisha
uwasilishaji wa mihadhara ambayo imekuwa ikiakisi mambo ya kiongozi huyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.